Wafungwa kuwezeshwa baada ya kifungo

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 05:22 PM Mar 12 2025
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (wa tatu kulia), akipokea maelezo
Picha: Idda Mushi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (wa tatu kulia), akipokea maelezo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ameahidi kuwa wizara hiyo itakaa meza moja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, ili kuona namna watakavyoweza kuwawezesha mitaji wafungwa wanaomaliza vifungo vyao gerezani, huku wakiwa tayari wana ujuzi unaotambulika.

Bashungwa alisema hayo katika Gereza la Mtego wa Simba, lililopo Mkambalani, wilayani Morogoro wakati akizindua programu ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, kwa wafungwa walio magerezani.

Pia aliwatunuku vyeti vilivyotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa wafungwa 201 wa magereza ya mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Arusha waliohitimu stadi nane za urekebu katika fani mbalimbali.

Katika uzinduzi huo uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Gereza la Mtego wa Simba, na kukamilika kwake kutagharimu Sh. milioni 314.8.

Wafungwa kuwezeshwa baada ya kifungo
Bashungwa amesema uzinduzi huo, umeanza kwa magereza ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Mashariki na utaendelea kwa kanda zingine.

Amesema wakati akipita kuona bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wafungwa hao, zikiwamo bidhaa za mikono, mmoja wa wafungwa wa kike alimwomba wasaidiwe suala la mitaji pindi wakitoka magerezani, ili wakatumie vyema ujuzi wao kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine.

"Wakati sisi na TAMISEMI tukikusudia kufanyia kazi mchakato huu, ili ikibidi zile asilimia 10 za halmashauri zinazotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ziende na kwa wafungwa hawa wenye ujuzi wanaomaliza vifungo.

“Lakini na wewe CGP (kKamishna Jenerali wa Magereza) unaweza kufanya kitu kwa ama kuanzisha mfuko, ili hizi bidhaa wanazotengeneza zikiuzwa, fedha ziingie kwenye mfuko na wakimaliza kifungo kila mmoja apewe chake akaanzie maisha,” alishauri Bashungwa.

Amewataka kutokata tamaa kwavile wapo Gerezani, kwani Rais Samia Suluhu Hassan, ameon aje na mawazo mazuri ya kuwasaidia kuwa raia wema na wanaojitegemea.

"Hata mimi Babu yangu alikuwa mfungwa hapo zamani, lakini alikubali kurekebishika kupitia program za urekebu magerezani na akawa fundi mzuri, amejenga shule, mahakama, zahanati na majengo mengine mengi kijijini, ukimuuliza yeyote anajua.

“Leo hii mjukuu wake ni waziri, hata ninyi msikate tamaa, mna nafasi ya kubadilika na kuwa watu wema na wanaoheshimika,” amesisitiza Bashungwa.

Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Katungu, alisema licha ya elimu ya urekebu wanayowapa wafungwa magerezani, ikiwamo kwenye masuala ya kilimo, mifugo, ujenzi, ususi, uvuvi na utengenezaji samani, wameendelea kutoa ujuzi na kuruhusu wafungwa kujiendeleza kimasomo ambapo wapo walio vyuo vikuu, elimu ya sekondari na elimu ya msingi.

Wafungwa kuwezeshwa baada ya kifungo
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasole, akasema kupitia program hiyo, wameshawafikia watu 23,674 wakiwamo waliopitia vyuo vya urekebishaji yaani Magereza.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Dk. Mwakahesya Uswege, akizungumzia program hiyo iliyoanza Mei 3, mwaka jana, alimesema iliwalenga wafungwa wenye umri wa chini ya miaka 50 na waliopata ujuzi wa zaidi ya miaka mitatu wakiwa Gerezani.

Anasema wafungwa 212 walifanyiwa usahili na 201 Sawa na asilimia 94.8 walifaulu na hivyo kustahili kupewa vyeti Katika fani za  Ujenzi, ufundi magari, uundaji na uchomeleaji, u meme wa majumbani, upishi, useremala, ubunifu na ushonaji nguo na ufundi Bbomba.

"Tunaamini wakirudi uraiani watakwenda kujiajiri wenyewe na kuajiriwa,kupata kipato, kuondokana na tabia ya kurudia makosa na jamii itafaidika kwa kupungua kwa uhalifu,” amesema Dk. Uswege.

Mafunzo hayo yamegharimiwa na serikali kupitia Jeshi la Magereza, kwa kila mfungwa aliyefanyiwa tathmini Kulipiwa VETA na NACTE hugharamiwa shilingi 122,000 kati ya mahitaji ya shilingi 235,000 na gharama zingine zimetolewa punguzo na VETA.