Kilichomuua aliyekuwa Mbunge Moshi Mjini hiki hapa...

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:33 PM Mar 12 2025
news
Picha: Godfrey Mushi
Mwili wa Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini (CCM), John Mwanga (78) ukiwa kwenye jeneza.

SIMANZI na vilio, vimetawala katika Kijiji cha Sisa Maro kilichopo Kata ya Okaoni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya mwili wa Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini (CCM), John Mwanga (78), kuwasili kijijini kwao kwa ajili ya maziko.

Mwanasiasa huyo, alikuwa Mbunge wa kwanza wa jimbo hilo, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Vyama Vingi nchini uliofanyika mwaka 1995.

Mwanga, alifariki dunia Machi 4 mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Selian iliyoko Jijini Arusha, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Amezikwa leo, Machi 12, 2025 katika makaburi ya familia yao yaliyoko Kibosho, Kijiji cha Sisa Maro, Kata ya Okaoni, Jimbo la Moshi Vijijini.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransico Kisaveri Mkombole, Padri Evarist Kawawu, aliyeongoza ibada hiyo, amesema marehemu, John  Mwanga, anapaswa kuombewa ili akapate pumziko la milele katika awamu ya pili ya safari yake.

Akisoma wasifu wa marehemu John Mwanga, mtoto wake, Imani Mwanga, amesema baba yake enzi za uhai wake, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (BP) na sukari.

Mwaka 2023, Mwanga, aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa moyo uliomsababisha kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Mwaka 1994/1995, mwanasiasa huyo alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uhusiano wa Mambo ya Nje, na mwaka 1991/1993, alikuwaMjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC).

Mwanasiasa huyo, ameacha mjane Aikael Moshi, watoto tisa, wajukuu 30 na vitukuu vitano.