Lissu: Sijaahidi chochote ambacho hakitekelezeki

By Enock Charles , Nipashe
Published at 01:05 PM Mar 12 2025
MWENYEKITI wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu
PICHA: MTANDAO
MWENYEKITI wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu

MWENYEKITI wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amesema mambo yote aliyoahidi wakati wa kampeni zake za kuwania Uenyekiti wa chama hicho ikiwamo suala la ruzuku na ukomo wa madaraka yanatekelezeka.

Akizungumzia utaratibu wa kugawanya mapato ya chama hicho ambao aliahidi kuubadilisha wakati anaomba kura, Lissu alisema Baraza Kuu la CHADEMA, litatengeneza mwongozo wa mgawanyo wa mapato hayo.

"Sijaahidi chochote ambacho hakitekelezeki. Suala la mgawanyo wa mapato linatekelezeka kabisa. Suala la ukomo wa madaraka linatekelezeka kabisa.”alisema Lissu

“Tunataka kwamba mwanachama anayelipia ile kadi ya platinum ya Sh. 200,000, kwa mfano, ajue kwamba katika hiyo fedha, kiasi fulani kitakwenda kwenye shughuli za makao makuu, kwenye shughuli za kanda, mkoani, wilayani, majimboni, ijulikane kabisa.”

“Ijulikane kama ambavyo zoezi hili la kuandikisha wanachama kidigitali ambalo tumetengeneza utaratibu ambao mawakala ambao wanatafuta wanachama wapya, katika kila Sh. 2,500 wanarudishiwa Sh. 500," alisema Lissu.

Alisema, Baraza Kuu litakapokutana, watapeleka mapendekezo ya maeneo mengine mengi yanayohitaji kufanyiwa marekebisho kwa kutengenezewa miongozo.

"Inabidi uelewe namna ya kufanya uamuzi kwenye chama kama CHADEMA. Kuna uamuzi ambao unahitaji utaratibu kama huo utengenezwe, Ni ama zitungwe kanuni mpya, itungwe miongozo mipya au ya zamani ibadilishwe. Hii ni kazi inayofanywa na Baraza Kuu.

"Kama mapendekezo hayo yanahitaji mabadiliko ya Katiba pamoja na ukomo wa madaraka, hiyo inahitaji mabadiliko ya Katiba ya chama ambayo inabadilishwa na mkutano mkuu wa chama," alisema.

Lissu alisema Baraza Kuu la chama hicho huwa linakutana mara moja kwa mwaka na kwamba watakapoitisha kikao cha baraza hilo ndipo watakapopeleka mapendekezo kuhusu mgawanyo wa fedha za chama hicho.

Kuhusu "Tone kwa Tone", Lissu alisema wanaamini wakienda nayo vizuri, itawakwamua na kuwafikisha mahali pazuri kwa ajili ya kusaidia kuendesha shughuli za chama hicho.

"Kwa ukarimu wa watanzania, itatusaidia. Nchi hii kwa kawaida utamaduni wa kuchangia shughuli za siasa huwa haupo. Wananchi huwa wanategemea kwamba 'wewe mwanasiasa unayetaka kuwa mbunge, wewe ndiwe utupe fedha kwa sababu ukishapata nafasi hiyo, unakwenda kwenye utajirisho halafu sisi unatuacha'.

"Sasa sisi tunajaribu kuleta utamaduni mpya. Tunawaambia wananchi wetu kwamba 'sisi hatuna fedha za kuendesha shughuli za hiki chama, hiki ni cha kwenu, ili tufanye kazi ambayo mnataka tuifanye kila siku, tunahitaji fedha'. Ni utamaduni mpya lakini kwa hicho tu ambacho tumekiona, kitatusaidia," Lissu alisema.

Wiki iliyopita, chama hicho kilitangaza kuwa kupitia huo mkakati wake wa kukusanya fedha, mpaka kufikia Machi Mosi mwaka huu, kilikuwa kimekusanya Sh. milioni 64.

Chama hicho kiliahidi taarifa ya makusanyo ya fedha hizo zitakuwa zinatolewa kila baada ya siku saba kupitia kamati ndogo ambayo imeteuliwa kwa ajili ya kazi hiyo.