Kampuni ya Grumeti Reserves imetoa madawati 150 kwa shule tatu za msingi katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, ili kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi.
Mkurugenzi wa Raslimaliwatu na Mahusiano wa Grumeti Reserves, Martha Baare, alikabidhi madawati hayo kwa viongozi wa shule hizo Alhamisi Machi 6, 2025.
Shule zilizonufaika na msaada huo na kata zake zikiwa kwenye mabano ni Manyago (Kyambahi), Miseke (Manchira) na Mbilikiri (Sedeko) ambapo kila shule ilipatika madawati 50.
“Grumeti Reserves kama mdau wa maendeleo tumeleta madawati haya kwa wanafunzi wa shule hizi tukijua ni moja ya kipaumbele,” alisema Basare wakati wa makabidhiano ya madawati hayo.
Alisema kampuni yake itaendelea kutoa mchango wake kwa sekta ya elimu na kuwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili baadhi yao baadaye waajiriwe na Grumeti Reserves.
Aliwahimiza wananchi katika maeneo hayo kuunga mkono juhudi za serikali za uhifadhi endelevu katika ikolojia ya Serengeti ili serikali izidi kujikita katika kuboresha huduma za kijamii.
Viongozi wa kijamii, walimu na wanafunzi walieleza kufurahishwa na msaada huo na kuahidi kutumia madawati hayo kuleta matokeo chanya katika kuinua ufaulu.
“Grumeti Reserves hawakuleta madawati haya kwa ajili ya kukalia tu, bali tunahitaji matokeo mazuri ya ufaulu wa wanafunzi. Sisi kama wasimamizi tutatimiza wajibu wetu,” alisema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Manyago, Okayo Misolo.
Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbirikiri, Hamisi Musoma, aliishukuru kampuni ya Grumeti Reserves kwa msaada wa madawati ambayo yatakuwa chachu kwa mafunzo kwa wanafunzi.
“Tunashukuru na kuahidi kwamba tutayatunza ya kuyatumia kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Wanafunzi katika shule zilizopatiwa madawati ‘walivaa’ nyuso za furaha kuonesha kuwa yatawasaidia katika mazingira ya kujifunza.
Katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Manchira, Jose Stanslaus Kitenena, aliahdi kwamba wananchi watendelea kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi na utalii kwa kumuunga mkono mwekezaji wa Grumeti Reserves.
“Tunafurahi kusikia mpo na mnatambua jamii kwa kuwafadhili watoto kupata elimu,” alisema.
Grumeti Reserves ni kampuni ya utalii iliyowekeza kwenye mapori ya akiba Ikorongo/ Grumeti na Hifadhi ya Jamii ya Ikona. Lakini pia, ni mdau wa maendeleo katika vijiji vinavyopakana nayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED