JUKWAA la TCF lataka wananchi kutoa taarifa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 05:33 PM Mar 11 2025
Sarah Masenga, Ofisa Habari wa Foundation For Civil Society(wa katikati mwenye nguo nyeupe), akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani), kuelekea maadhimisho ya siku ya hai za mtumiaji Machi 15 mwaka huu
Picha: Elizabeth Zaya
Sarah Masenga, Ofisa Habari wa Foundation For Civil Society(wa katikati mwenye nguo nyeupe), akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani), kuelekea maadhimisho ya siku ya hai za mtumiaji Machi 15 mwaka huu

JUKWAA la Watumiaji Tanzania (TCF), kwa kushirikiana na Foundation For Civil Society (FCS), wamewaomba wananchi kutoa taarifa kwa taasisi zinazowatetea pale wanapopata madhila wakati wanapatiwa huduma mbalimbali za kijamii.

TCF imetoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya haki za mtumiaji ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika Machi 15 mwaka huu.

Katibu wa Jukwaa hilo, Debora Mlingo, alisema bado hakuna mwamko kwa wananchi wa kutumia vyombo hivyo vinavyowatetea kutoa taarifa ya madhila wanayokutana nayo wakati wa kupata au kufuata huduma kwenye taasisi mbalimbali nchini.

Alisema ni vema wakatumia taasisi hizo ili ziwasaidie kupata haki zao za msingi kwa kuzingatia haki na taratibu za kisheria.

“Taasisi hizi zimeanzishwa kwa lengo la kulinda haki za watumiaji na kuhimiza matumizi salama na endelevu ya huduma na ni fursa ya kipekee kwa wananchi kupata elimu kuhusu haki zao,”alisema Debora.

“Lakini shida kubwa tunayoiona, wananchi au watumiaji wengi wa huduma, hawana mwamko wa kuripoti matukio au madhila wanayokutana nayo kwenye harakati za kutafuta huduma.”

Kadhalika, alisema pia ni wakati kwa taasisi mbalimbali zinanazotoa huhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati pale wanapozihitaji kwa wananchi kwa sababu ni haki yao kuipata kulingana na uhitaji wao.

Ofisa Habari wa FCS, Sarah Masenga, alisema  lengo lao wanataka kuona wananchi wanatatuliwa changamoto na malalamiko yao yote katika sehemu na taasisi mbalimbali wanakozifuata.

“Tunataka wananchi wafaidike kwa sababu ndio wadau wakubwa na muhimu sana wa maendeleo, kuna mwananchi ambaye anafanya biashara za nafaka, mwingine ni mama ana biashara zake za mbogamboga, wote hao tunataka wapate huduma stahiki kwenye shughuli zao nak ama kuna madhila wanakutana nayo tuyafahamu.

“Na wanapokutana na madhila hayo, wafahamu zipo taasisi  wanatakiwa kuzifikia au kwenda ili ziwasaidie kufikisha malalamiko yao na wapate haki zao, wengine hawajui wanatakiwa waende wapi pale wanapopata changamoto, kwa hiyo jukwaa la TCF linafanya kazi hiyo, na kikubwa wafahamu haki zao na wazipate,”alisema Sarah.