CHADEMA kuanza kukusanya taarifa za waliopotea mazingira ya kutatanisha

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 09:18 AM Mar 11 2025
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche.
Picha: Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kuendesha zoezi la kukusanya taarifa za watu wote walioripotiwa kupotea kwa mazingira ya kutatanisha nchini kote.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, aliandika kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X kwamba chama hicho kitalazimika kuorodhesha taarifa hizo kutoka kila kona ya nchi ili hatua zaidi zichukuliwe.  

Heche alieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kupitia matukio ya utekaji na mauaji ambayo yamekuwa yakishamiri kwa miaka ya hivi karibuni.  

"Kwa maana hii, chama chetu katika kila wilaya, kata na kitongoji kitalazimika kukusanya na kuhifadhi taarifa hizi kwa kina na kuziwasilisha makao makuu ya chama ili hatua zaidi zichukuliwe," aliandika Heche.  

Aliongeza kuwa kwa sasa vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kwa wingi matukio ya watu kutekwa, kupotea au kuuawa katika maeneo mbalimbali nchini.  

"Hakuna siku inayopita bila kupokea taarifa za mtu kutekwa, kupotea au kuuawa katika sehemu fulani," alisema Heche.  

Kauli ya Rais Samia Kuhusu Vitendo vya Utekaji 


Julai 20, 2024, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza na machifu katika Uwanja wa Chamwino, Dodoma, alikiri kuongezeka kwa vitendo vya utekaji nchini. Alisisitiza kuwa jamii inapaswa kushirikiana na serikali kuvitokomeza badala ya kufumbia macho.  

"Tukizungumza kuhusu utekaji, ukiuliza katekwa nani, unasikia mtoto alijiteka mwenyewe akapiga simu kwao wakatoa pesa, huku mama kamtekesha mwanaye ili baba atoe pesa—yaani mambo ya drama tu," alisema Rais Samia.  

Hata hivyo, alikosoa jinsi suala hilo linavyoripotiwa na vyombo vya habari, akisema "lakini vinavyoandikwa kwenye magazeti ni kama serikali imelala na watu wanatekwa ovyo. Haya mambo yanatokea katika jamii yetu, naomba tusiyafumbie macho."  

Ukimya wa Serikali Kuhusu Idadi ya Waliotekwa  

Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka serikalini kuhusu idadi kamili ya watu wanaodaiwa kutekwa au kupotea kwa nia ovu. Taarifa ya mwisho iliyotolewa kuhusu matukio hayo ilikuwa tarehe 3 Julai 2024 jijini Dar es Salaam.  

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, alizungumzia suala hilo wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zuberi, kiitwacho Mmomonyoko wa Maadili: Nani Alaumiwe?  

Masauni alieleza kuwa matukio ya utekaji ambayo mara kwa mara yamekuwa yakitajwa, wanasiasa wamekuwa wakiyahusisha na serikali pamoja na vyombo vya usalama vilivyopewa dhamana ya kulinda wananchi. Kwa mujibu wa Masauni, tangu Januari hadi Julai 2024, matukio ya utekaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana hayakuzidi manane.  


ACT Wazalendo Watoa Kauli  


Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, ambaye pia ni muathirika wa utekaji, alisema serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa raia wake. Alisisitiza kuwa vitendo vya utekaji kwa mwaka 2024 viliongezeka kwa kiwango kikubwa.  

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio la utekaji wake, Nondo alisema licha ya matukio hayo kushamiri, vyombo vya dola vimeshindwa kutoa taarifa rasmi kuhusu hali hiyo na juhudi za kuikemea.