Katibu Mkuu wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO), Daniel Mkinga, amesema kikao kati ya NETO na mawaziri watatu, kilichopangwa kufanyika Machi 10, 2025, kimeahirishwa hadi Machi 12, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkinga, NETO imepokea taarifa kutoka Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ikieleza kuwa kikao hicho kimesogezwa mbele.
"Ndugu wananchi, tumepokea taarifa kutoka ofisi ya Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora juu ya kuahirishwa kwa kikao kilichopangwa kufanyika Jumatatu, tarehe 10 Machi 2025, na kusogezwa hadi Jumatano, tarehe 12 Machi 2025," alisema Mkinga.
Mkinga alibainisha kuwa nafasi 15 za wawakilishi zimetolewa kwa ajili ya kikao hicho, ili kutoa fursa ya kujadili kwa kina hoja na mapendekezo ya NETO.
"Kutokana na uchache wa nafasi, viongozi wa kitaifa wa NETO pamoja na wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali watahudhuria kikao hicho," aliongeza.
Pamoja na mabadiliko hayo, NETO imekubali kusubiri hadi tarehe iliyopangwa, ingawa baadhi ya viongozi tayari walikuwa wamewasili Dodoma, huku wengine wakiwa njiani kuelekea kuhudhuria kikao hicho.
"Tunaomba wanachama wa NETO na wananchi kwa ujumla kuwa na uvumilivu. Hivyo, NETO haitachukua hatua nyingine yoyote hadi baada ya kikao hicho," alisema Mkinga.
Aidha, NETO imetoa tahadhari kuhusu uwepo wa akaunti nyingi kwenye mitandao ya kijamii zinazotumia jina la NETO, ambazo zinadaiwa kusambaza maudhui chonganishi yenye lengo la kuchafua taswira, dhamira na malengo ya umoja huo.
"Ikumbukwe kuwa NETO itaendelea kupigania haki za walimu wote wasio na ajira nchini bila kuweka mbele maslahi binafsi," alisema Katibu Mkuu huyo.
Awali, Machi 3, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alitangaza kuwa mawaziri watatu wangekutana na NETO Machi 10, 2025, kwa ajili ya kujadili hoja zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED