Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimezindua rasmi Mtandao wa Uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu Mahali pa Kazi Nchini (NBDN), hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika uzinduzi huo leo, Mtendaji Mkuu wa ATE,Suzanne Ndomba-Doran, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, waajiri, na mashirika mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha fursa sawa za ajira.
Ndomba-Doran ameeleza kuwa ATE kwa kushirikiana na Sightsavers International inatekeleza mradi wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, huku ikiwahamasisha waajiri kuandaa mazingira jumuishi.
Katika mradi huo, waajiri wanajengewa uelewa kuhusu ujumuishaji wa watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (UNCRPD).
Kwa sasa, kampuni sita zimeshajiunga na mtandao huo, zikiwemo Standard Chartered Bank, ALAF, Serengeti, G4S, Swissport, na Reet. ATE pia hutambua waajiri wanaofanikisha ujumuishaji kwa kutoa tuzo maalum za waajiri bora katika kipengele cha utofautishaji na ujumuishaji.
Katika juhudi za kukuza uongozi jumuishi, ATE inaendesha programu ya "Mwanamke Kiongozi" inayolenga kuwajengea uwezo wanawake, wakiwemo wenye ulemavu, kushiriki katika nafasi za maamuzi.
Ndomba-Doran amemalizia kwa kushukuru serikali kwa juhudi zake katika kukuza uchumi na kuahidi kuwa ATE itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa jumuishi kwa watu wote.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline Khamati Mugalla, ameipongeza ATE na wadau wake kwa kuanzisha Mtandao wa Uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu Mahali pa Kazi (NBDN).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mugalla amesema kuwa ujumuishaji wa watu wenye ulemavu ni sehemu ya juhudi za ILO katika kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza ubaguzi na kuboresha mazingira ya kazi kwa makundi yote maalum.
Ameeleza kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana, bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili watu wenye ulemavu katika ajira, ikiwemo mitazamo hasi na mazingira yasiyo rafiki kazini.
ILO kupitia Mtandao wa Kimataifa wa Biashara na Ulemavu imekuwa ikiunga mkono kampuni zinazojitahidi kuunda mazingira jumuishi kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu.
Mugalla amehimiza kampuni kuzingatia Mwongozo wa ILO wa Ujumuishaji wa Watu Wenye Ulemavu kazini, ambao unatoa viwango na nyenzo za kuwezesha biashara kujenga mazingira jumuishi. Aidha, alitoa wito kwa serikali kuridhia Mkataba wa ILO Na. 159 ili kuwezesha utekelezaji wa sera madhubuti za ajira kwa watu wenye ulemavu.
Amemalizia kwa kusisitiza kuwa ILO itaendelea kushirikiana na ATE, TUCTA na wadau wengine kuhakikisha kuwa jukwaa la NBDN linafanya kazi kwa ufanisi, likichangia maendeleo endelevu na haki za watu wenye ulemavu katika soko la ajira.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, ameeleza furaha yake kwa kuzinduliwa kwa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika Biashara (NBDN), akisisitiza kuwa serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika ajira unatekelezwa kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Nderiananga amefikisha salamu kutoka kwa Rais Samia na Wizara husika, akipongeza juhudi za Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na shirika la Sightsavers katika kuanzisha mtandao huo.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika jamii na katika sekta ya ajira. Ni muhimu siyo tu kuwapatia ajira, bali pia kuhakikisha ubora wa ajira wanazozipata. Watu wenye ulemavu ni waaminifu, wachapakazi na wanaotegemewa, hivyo waajiri wanapaswa kuwapa nafasi zaidi,” amesema Nderiananga.
Amewataka waajiri kusikiliza mahitaji ya watu wenye ulemavu, kuongeza juhudi za kuwaingiza katika nafasi mbalimbali za kazi, na kupunguza unyanyapaa unaowakabili katika mazingira ya kazi.
Aidha, amezipongeza kampuni za Standard Chartered Bank, Alaf, Serengeti Breweries Limited, Swiss Port, G4S, na Reet Tanzania kwa kuwa miongoni mwa waasisi wa mtandao huo nchini, akizihimiza kampuni nyingine kuiga mfano huo ili kuongeza fursa kwa watu wenye ulemavu.
“Tunataka kuona mabadiliko ya kweli katika ajira kwa watu wenye ulemavu. Serikali itaendelea kushirikiana na ATE na Sightsavers ili kuhakikisha kuwa mtandao huu unakuwa na matokeo chanya kwa jamii,” amehitimisha Nderiananga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED