Mwanakwaya wa Kanisa Katoliki Parokia ya Buhangija, Manispaa ya Shinyanga, Agatha Nyahuma (32), mkazi wa Bugayambelele, Kata ya Kizumbi, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana waliomtaka kwa vitu vyenye ncha kali katika maeneo ya mabega, mgongoni na mkono wa kulia.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12:30 asubuhi katika Mtaa wa SIDO, Buhangija.
Kwa mujibu wa Kamanda Mgani, marehemu alikuwa akitoka nyumbani asubuhi akielekea kwenye Misa ya Asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Buhangija, lakini alikutana na watu wasiojulikana waliomshambulia kwa visu na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
"Baada ya kushambuliwa, alianguka chini na wasamaria wema walimkimbiza katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi," alisema Mgani.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa SIDO, Emmanuel Kayange, amelaani vikali tukio hilo, akisema marehemu alikutwa na majeraha makubwa yanayoonyesha alichomwa kwa visu katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
"Tumesikitishwa na tukio hili, na tunaiomba serikali na vyombo vya ulinzi kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Kayange.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED