Apata 'ajali' angani akiwa kwenye ungo aangukia TANESCO

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 05:26 PM Mar 11 2025
Apata 'ajali' angani akiwa kwenye ungo aangukia TANESCO

Taharuki imetanda katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, baada ya mwanamke mmoja, ambaye jina lake halijafahamika, kukutwa akiwa uchi ndani ya ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa akisafiri kwa ungo (ushirikina) kutoka Masasi, mkoani Mtwara, akielekea wilayani Nyasa, lakini alijikuta akianguka katika eneo la ofisi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa usiku kuamkia Machi 11, 2025.

TUKIO LINAVYOSIMULIWA

Kamanda Chilya ameeleza kuwa baada ya mwanamke huyo kukutwa katika eneo la jengo la TANESCO na umati wa watu kuanza kukusanyika, uongozi wa shirika hilo ulitoa taarifa kwa Kituo Kikuu cha Polisi Songea.

Askari polisi walifika haraka eneo la tukio na kumkuta mwanamke huyo akiwa uchi wa mnyama, huku akiwa amejificha kwenye moja ya vyoo vya ofisi hizo. Baada ya mahojiano ya awali, maafisa wa polisi waliamua kumpeleka Hospitali ya Mkoa wa Songea (HOMSO) kwa uchunguzi zaidi ili kubaini hali yake ya kiafya, hasa ikiwa anatatizo la afya ya akili. Kwa sasa, amelazwa katika wodi namba nane akisubiri uchunguzi wa kitaalamu.

USHUHUDA WA WANANCHI

Tukio hilo limezua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa Songea, huku baadhi yao wakieleza kushangazwa na hali hiyo, ingawa serikali haitambui uwepo wa ushirikina.

Athumani Mohamed, mkazi wa Mtaa wa Ruvuma, amesema inadaiwa kuwa mwanamke huyo alipita karibu na Kanisa la Pentekoste REDMD (Walokole) ambapo alipoteza mwelekeo, na hatimaye akaanguka ndani ya uzio wa ofisi za TANESCO akiwa uchi huku usoni akiwa amepakaa unga.

Naye Asha Omari, mkazi wa Mtaa wa Mateka, ametoa wito kwa serikali na vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli kuhusu tukio hilo. Alipendekeza kuwa mwanamke huyo anapaswa kuwataja watu aliokuwa nao kwenye safari hiyo ili hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya vitendo vya ushirikina ambavyo vinakwamisha maendeleo ya jamii.

TAMKO LA HOSPITALI

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Songea, Dk. Magafu Majura, amesema kwa sasa yuko nje ya mkoa kwa shughuli za kikazi, lakini alithibitisha kuwa uchunguzi juu ya hali ya mwanamke huyo unaendelea na taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.