SWALI ambalo umma unajuliza ni Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, yuko wapi?
Swali hilo limezidi kuibua hisia nyingi baada ya kiongozi huyo aliyeongoza chama hicho kwa miaka 21 kutoonekana kwenye jukwaa lolote au vikao vilivyoitishwa na Mwenyekiti, Tundu Lissu.
Tangu Januari 22, mwaka huu, mara baada ya Mbowe kuhutubia Mkutano Mkuu wa CHADEMA kukubali matokeo yaliyompa ushindi Lissu, akiahidi ushirikiano hajaonekana wala kusikaka kokote.
Katika mkutano huo Lissu alimwambia Mbowe kuwa ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Kikao hicho cha kwanza cha uongozi huo mpya ni kile kilichoanza na kikao maalumu kilichopewa jina la ‘Retreet’ ambacho baada ya uongozi huo mpya kupatikana, ulijifungia ndani kwa zaidi ya siku saba kujadili namna ya kuendesha chama chao hicho na namna ya kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi.
Kwenye kikao cha kwanza, si Mbowe pekee ambaye hakushiriki, lakini hata Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, ambaye katika uchaguzi mkuu uliowapata viongozi hao wapya na yeye akigombania nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, naye hakushiriki.
Picha zilizosambazwa kwa umma na Kitengo cha Mawasiliano cha chama hicho Machi 11,2025 zilimuonyesha Wenye, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu kama Bon Yai ambaye pia alikuwa timu ya Mbowe wakati wa kampeni alikuwa miongoni mwa walioshiriki.
Aidha, wajumbe wengine kama Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi, Devota Minja, huku Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu hakushirikia lakini kwenye mitandao yake ya kijamii alisambaza picha kuwa yupo safarini Marekani.
Aidha, Mbowe hakuonekana kwenye kikao hicho, na hakuna taarifa iliyotolewa kwa umma.
Nipashe Digital ilitembelea mitandao ya kijamii hasa X ambako ndiko kiongozi huyo ili kuona alichoandika mara ya mwisho lakini haikufanikiwa kuzikuta akaunti zake
Machi 9,2025, Lissu alipofanya mazungumzo maalum na Nipashe Gazeti na Nipashe Digital alipoulizwa kuhusu mpango wa kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi Januari 21,mwaka huu, amesema jukumu hilo limekabidhiwa Baraza la Wazee CHADEMA.
Aidha, amethibitisha kuwa uchaguzi huo uliacha majeraha kwa pande zote na kukiri ulazima wa kuyaponya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED