SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imelipa siku mbili kuanzia leo Machi 12, 2025 hadi Machi 14, 2025 Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry.
CAF imefikia hatua hiyo baada ya kuufungia kwa muda Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam kutokana na eneo la kuchezea (pitch) kuendelea kupungua ubora wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 12, 2025 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, CAF imesema eneo hilo liboreshwe haraka kufikia viwango vinavyotakiwa ili kuepuka uwanja huo kufungiwa kwa muda mrefu.
“Ili kuondoa usumbufu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba kufikia Machi 14, 2025.
“CAF itafanya ukaguzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 20, 2025 ili kuona maboresho yaliyofanyika kabla ya kuamua kuuruhusu utumike au kuendelea kuufungia,” imeeleza taarifa hiyo.
Ikumbukwe kuwa, uwanja huo unatumiwa na Simba kwa mechi za kimataifa ikitarajiwa kucheza dhidi ya Al Masry hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao umepangwa kuchezwa Aprili 9, 2025.
Mbali ya mechi hizo za CAF, Uwanja wa Benjamin Mkapa umepangwa kutumika kwa ajili ya michuano ya CHAN itakayofanyika Agosti 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED