Prof. Issa Shivji ashusha nondo kuhusu Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:27 PM Mar 12 2025
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issa Shivji.
Picha: Mtandao
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issa Shivji.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issa Shivji, amesema kuwa ripoti ya tathmini ya namna redio zilivyoripoti Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, iliyotolewa na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), ilipaswa kuchambua mchakato mzima wa uchaguzi huo na kutoa mapendekezo sahihi.

Akizungumza leo Machi 12, 2025, wakati wa tathmini ya ripoti hiyo, Prof. Shivji amesema kuwa uchaguzi hauishii kwenye kampeni pekee, bali unajumuisha hatua zote muhimu kama uandikishaji wa wapigakura, utangazaji wa wagombea, kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza washindi rasmi.

Kwa maoni yake, ripoti hiyo haikuzingatia mchakato mzima wa uchaguzi, bali iligusa sehemu ndogo tu, jambo linalopunguza uhalisia wa tathmini hiyo. 

"Sababu zao wanazijua, lakini wasiniambie kwamba hawakuwa na fedha," amesema Prof. Shivji kwa msisitizo.

Masuala Muhimu Yaliyopuuzwa

Prof. Shivji ameeleza kuwa ripoti hiyo ilipaswa pia kugusia malalamiko yaliyotolewa na vyama vya upinzani kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa shule walio chini ya umri wa kupiga kura. 

"Tuliona video zikionesha watoto wakiwa katika sare za shule wakisubiri kuandikishwa kupiga kura. Hili ni jambo muhimu, kwani linahusiana na haki na uadilifu wa uchaguzi," amesema.

Amesisitiza kuwa kutokuzingatia suala hilo kunaathiri dhana ya uchaguzi huru na wa haki.  

"Unapowaandikisha vijana ambao hawajakidhi vigezo vya kupiga kura, unawafundisha kufanya mambo yasiyofaa tangu wakiwa wadogo," ameongeza.

Prof. Shivji pia ameeleza kushangazwa na ripoti hiyo kwa kutotathmini jinsi redio zilivyoripoti shutuma hizo. 

"Watafiti hawakutaja kama vituo vya redio vilitangaza, vilikuwa na mijadala au vipindi kuhusu shutuma hizi," amesema.

Kauli ya Jaji Warioba Haikuzingatiwa

Akinukuu maoni ya Jaji Joseph Warioba, ambaye alizungumzia uchaguzi wa 2024, Prof. Shivji ameeleza kuwa ripoti hiyo ilipaswa kuchambua kwa kina matamshi yake.

 "Jaji Warioba, ambaye si mwanachama wa chama cha upinzani, alitoa kauli nzito kwamba 'uchaguzi wa 2024 haukuwa tofauti na wa 2019, na kama hali hii itaendelea katika uchaguzi wa 2025, itahatarisha amani.' Kauli hii ilihitaji mjadala wa kina kutoka kwa watafiti," amefafanua.

Ameongeza kuwa watafiti walipaswa kuangalia kama redio zilifuatilia na kujadili mada hiyo kwa kina. "Uchaguzi huru unapaswa kuwa na mijadala ya wazi wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi. Hakuna siri katika uchaguzi, na ni jukumu la vyombo vya habari kuelimisha wananchi," amesisitiza.

Masuala ya Kuenguliwa kwa Wagombea

Kwa mujibu wa Prof. Shivji, ripoti hiyo imeeleza kuwa baadhi ya wagombea walienguliwa kwa sababu ya kushindwa kujaza fomu kwa usahihi. Hata hivyo, baadaye, Katibu Mkuu wa CCM alizungumzia suala hilo, na muda wa kukata rufaa ukaongezwa, ambapo wagombea 5,500 waliorudishwa kwenye kinyang'anyiro.

"Swali ni, kama walishinda rufaa na wakarejeshwa, maana yake ni nini? Kwa nini walirejeshwa? Hili ni jambo muhimu ambalo watafiti walipaswa kulichambua kwa kina," amesema.

Uandishi wa Habari za Uchunguzi Umekosekana

Prof. Shivji pia ameeleza kushangazwa na ripoti hiyo kwa kutotilia mkazo umuhimu wa uandishi wa habari za uchunguzi.

 "Nilishangaa kuona kuwa hakukuwa na kigezo cha uandishi wa uchunguzi. Tangu nilipokuwa Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), nimeona waandishi wengi wa habari hawajafundishwa ujasiri wa kufanya uchunguzi wa kina. Kuna mambo mengi yanayotokea nchini, lakini vyombo vya habari havileti undani wake," ameeleza.

Kwa maoni yake, tathmini hiyo ni zaidi ya chapisho la kawaida; ni zana muhimu ya kufundishia. Amesisitiza kuwa ripoti kama hizo zinapaswa kuwa na uchambuzi wa kina unaowafanya wasomaji wake kutaka kuisoma mara kwa mara.

Mapendekezo kwa Ripoti Zijazo

"Natarajia ripoti ya mwaka 2025 iwe tofauti. Mbali na kutoa taarifa, ijumuishe makala za uchambuzi wa kina kuhusu takwimu na matukio muhimu badala ya kuwa na orodha ya pointi pekee," amehitimisha Prof. Shivji.