Serikali yaanza uhakiki wa anwani za makazi Mbeya

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 03:42 PM Sep 24 2025
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda.

Serikali imeanza zoezi la kuhakiki na kuboresha anwani za makazi jijini Mbeya ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na huduma mbalimbali zinazopatikana kupitia mfumo huo.

Zoezi hilo linafanywa na maofisa wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa mitaa, ambapo mafunzo yametolewa kwa watendaji hao kabla ya kuanza kuhamasisha wananchi.

Ofisa Tehama wa Kitengo cha Anwani za Makazi, Rehema Chillo, amesema zaidi ya siku 14 zitatumika kuhakiki anwani hizo jijini Mbeya pekee. Amesema wakati wa oparesheni ya mwaka 2022, zaidi ya anwani 480,000 ziliingizwa kwenye mfumo lakini kutokana na mabadiliko ya ujenzi na umiliki, uhakiki unahitajika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu, Josephine Mwaijande, alisema kasoro zilizojitokeza awali zitatatuliwa wakati huu, ikiwemo baadhi ya nyumba na mitaa kurukwa kutokana na haraka ya waajiriwa waliokuwa wakikusanya taarifa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, alihimiza wananchi kushirikiana na maofisa ili serikali iwe na kanzidata sahihi, akibainisha kuwa mfumo huo una lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo huduma za afya.