Kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kisiwa cha Uzi, Mkoa wa Kusini Unguja, kuhusu changamoto ya usafiri kutokana na kutokuwepo kwa daraja, sasa kimepata ufumbuzi baada ya serikali kuanzisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilomita 2.2.
Ujenzi wa daraja hilo unaoendelea umekwishafikia asilimia 62 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu. Kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Kisiwa cha Uzi kimezungukwa na bahari na misitu ya mikoko, kikijulikana kwa mandhari yake ya kipekee na utulivu. Ujenzi huo umetajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha maendeleo ya visiwa vidogo.
Kwa sasa, wakati maji ya bahari yanapotoka, kisiwa hicho kinaweza kufikiwa kwa miguu au kwa gari kupitia barabara ya mawe inayounganisha kijiji cha Unguja Ukuu. Hata hivyo, maji yanapopanda, wakazi na wageni hutegemea mitumbwi au boti kufika kisiwani.
Daraja jipya linatarajiwa kuondoa changamoto hizo na kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji kisiwani humo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED