Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewataka wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlowo iliyopo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kutoa taarifa za wanafunzi wenzao ambao wamekuwa wakizurura na kucheza mitaani pindi watokapo shuleni ili waepukane na kufanyiwa vitendo vya ukatili wanavyoweza kukumbana navyo mitaani na njiani.
Kauli hiyo ilitolewa Aprili 22, 2025 na Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nicholas Livingstone ambapo amesema kitendo cha wanafunzi kucheza mtaani pindi watokapo shule kinaweza kuwapelekea kufanyiwa vitendo vya ukatili kitendo na unyanyasaji dhidi yao ambacho kitawarudisha nyuma kimasomo na kushindwa kutimiza malengo ya masomo na maisha yao ya baadae.
Aidha, ACP Livingstone amewataka wanafunzi hao wanapowaona wenzao wanacheza na kuzurura mtaani pindi watokapo shuleni watoe taarifa kwa walimu au wazazi wao ili waweze kutatua tatizo hilo kwa haraka.
Pamoja na mambo mengine, ACP Livingistone amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza na kuwatii wazazi na walimu ili waendelee kuwa na maadili mema katika jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED