Licha ya juhudi mbalimbali za kuleta amani, hali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) bado haijatulia huku mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23 yakiendelea. Tayari miji kadhaa mashariki mwa nchi hiyo, ikiwemo Goma, Bukavu na Nyabibwe, iko chini ya udhibiti wa waasi.
Katika hatua nyingine kubwa, serikali ya Rais Félix Tshisekedi imepiga marufuku shughuli zote za chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) kinachoongozwa na rais wa zamani Joseph Kabila. Pia, imeamuru kutaifisha mali zake, ikimtuhumu Kabila kushindwa kulaani machafuko yanayofanywa na M23 na kuhusishwa moja kwa moja na kundi hilo.
Kulingana na taarifa rasmi ya Aprili 19, 2025, serikali imesema kurejea kwa Kabila nchini humo kupitia jiji la Goma—eneo linalodhibitiwa na M23—ni kitendo kisichoeleweka. Serikali imetangaza kufungua mashitaka dhidi yake kwa tuhuma za usaliti kwa taifa, huku ikizuia usafiri wa washirika wake wote.
Kabila, ambaye alikuwa uhamishoni Afrika Kusini tangu 2023, aliongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Désiré Kabila. Taarifa zinasema amerudi nchini kwa nia ya kusaidia kutatua mgogoro unaoendelea.
PPRD haijatoa tamko rasmi kuhusu marufuku hiyo, huku msemaji wa Kabila akisema kuwa atalihutubia taifa hivi karibuni. Msemaji wa M23 naye hakuthibitisha wala kukanusha uwepo wa Kabila mjini Goma.
Uhusiano kati ya Kabila na Rais Tshisekedi umekuwa wa mashaka tangu alipoondoka madarakani, huku tuhuma zikiendelea kuwa uchaguzi wa 2018 ulifanyika kwa makubaliano ya pande zote mbili dhidi ya Martin Fayulu, anayesemekana kushinda kihalali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED