Watanzania: Changieni damu kwa wahitaji

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 03:10 PM Apr 22 2025
Watanzania wahimizwa kuchangia damu kwa wahitaji
Picha: Idda Mushi
Watanzania wahimizwa kuchangia damu kwa wahitaji

WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuchangia damu kwa hiyari, kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo, ili kuokoa wahitaji wakiwamo majeruhi, wajawazito na watoto.

Aidha wananchi wametolewa hofu kuwa kuchangia damu, kwamba hakuna athari zozote za kiafya, ikiwamo kudhoofu ama kutoa mwanya kwa mlipuko wa magonjwa mbalimbali.

Mratibu wa Damu Salama kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Ileme Wilson, amesema hayo katika Kata ya Mzinga, manispaa ya Morogoro wakati wa uchangiaji damu kutoka kwa vijana 110 wenye umri wa kati ya miaka 17 hadi 25.

Vijana hao walio kwenye kambi yao maalum, ni waliowahi kuishi ama kufanya kazi mitaani, ambao kwa sasa wanahifadhiwa, kuendelezwa kitaaluma katika ngazi za elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu maeneo mbalimbali nchini, huku wengine wakifuzu kutoka mtandao wa ‘Safina Street Network’.

Dk. Ileme Wilson, amesema hospitali hiyo, inatumia takribani uniti 15 hadi 20 kila siku, kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga, wajawazito, wanafanyiwa upasuaji, wenye selimundu, majeruhi, hivyo mahitaji ni makubwa siku hadi siku.

"Ikumbukwe damu ni bure, haiuzwi, kwa hiyo hatuwezi kuwa nayo kama watu hawatajitolea kwa hiyari, ili kuokoa maisha ya wahitaji, tunawashukuru sana vijana hawa wa mtandao huu.

“Msaada huu mfululizo, kila mwaka kwa mwaka wa nne sasa wamekuwa wanachangia damu kwa hiyari," amesema mratibu huyo.

Watanzania wahimizwa kuchangia damu kwa wahitaji
Abasi Mwinuka, Joseph Matreka na Selemani Nazareth, kwa nyakati tofauti wamesema kwa mwaka wa nne sasa wanachangia damu na hawajapata madhara yeyote kiafya.

Wanaona ni tukio la thawabu kiimani, lakini ni faraja kumwokoa mhitaji ambaye anaweza kupoteza maisha kwa kukosa damu.

Mkurugenzi wa Huduma kutoka Safina Street network, Nicolaus Duma, amesema wamekuwa wakihudumia watoto wanaowapata kutoka mitaani wakiwamo watoto.

"Tunaomba sana serikali itusaidie kama wadau, tuna jukumu kubwa kuwahudumia hawa watoto zaidi ya 300, tunamuombea Rais Samia Suluhu Hassan, atuangalie.”