Maelfu ya Wacomoro wanufaika kambi ya madaktari bingwa wa Tanzania

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 AM Apr 22 2025
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI na taasisi ya Global Medicare walikabidhi ripoti serikalini ya  kambi ya siku 7 iliyofanyika nchini Comoro.
Picha: Mwandishi Wetu
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI na taasisi ya Global Medicare walikabidhi ripoti serikalini ya kambi ya siku 7 iliyofanyika nchini Comoro.

Kambi ya matibabu iliyofanywa na madaktari bingwa wa Tanzania nchini Comoro imekuwa ya mafanikio makubwa kwani wananchi zaidi ya 2,270 waliokuwa na changamoto za kiafya walipata tiba.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge wakati wa kukabidhi ripoti ya kambi hiyo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk  Seif Shekilage.

Ripoti ya kambi hiyo iliyofanyika Novemba mwaka jana iliwasilishwa sanjari na andiko la pendekezo la maandalizi ya ziara ya ujumbe wa sekta ya afya kutoka Comoro nchini Tanzania Iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel.

Madaktari hao bingwa walitoka Taasisi ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), JKCI, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Alisema  kati ya wagonjwa 2,270 waliopatiwa matibabu 221 walipewa rufaa kuja kutibiwa kwenye hospitali za Tanzania na wengi wameshafika.


“Asilimia 30 ya hao wameshafika kutibiwa kwenye hospitali za Tanzania na wapo waliokuwa na shida ya umeme wa moyo tumeshawawekea peacermaker tumefanikiwa kuokoa maisha yao,” alisema

1

Alisema Rais wa Comoro alishukuru kwa uamuzi wa serikali ya Tanzania kuruhusu madaktari wake kwenda kuweka kambi ya wiki moja ambapo wananchi wenye shida mbalimbali walipatiwa matibabu ya kibingwa.


“Ile kambi ya matibabu ilikuwa ya mafanikio makubwa sana na imeiongezea Tanzania sifa ya kuwa kitovu cha utalii tiba hapa Afrika na mbali na fursa ya matibabu ile kambi imeibua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wacomoro wengi kufahamu vyema Tanzania na kuanza kufanyabiashara na wenzao wa hapa,” alisema


Dk Kisenge alisema Tanzania inatarajia kupata ugeni mkubwa wa viongozi wa nchini Comoro wakiongozwa na Wizara ya Afya ya nchini humo ambao watakuja kuangalia uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwenye sekta ya afya.

 Mkurugenzi Mkuu wa GlobalMedicare, iliyoratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na JKCI,  Abdulmalik Mollel, alisema kwenye kambi hiyo walikuwa wanakuja zaidi ya watu 1,000 hali inayoonyesha kuwa kuna mahitaji makubwa ya madaktari.

“Ili wale 1,000 waje ilikuwa lazima wapewe taarifa kwa hiyo sisi Globalmedicare tuliweka mkazo kwenye elimu kwa umma ili watu wafahamu huduma zinazotolewa, kule watu hawajui MOI au JKCI sisi Global Medicare ilikuwa kazi yetu kuwaeleza huduma wanazotoa,” alisema
“Mfano kwa mtu mwenye saratani sisi ilikuwa wajibu wetu kuwaeleza sehemu ya kwenda kutibiwa hapa Tanzania, kama ni moyo tuliwaeleza waende JKCI kwa shida zinazohitaji rufaa,” alisema Mollel


Aliishukuru serikali ya Comoro kwa namna ilivyowajali madaktari hao bingwa ambao walipokelewa kama wageni mashuhuri VIP na kwamba hawakufanyiwa hata ukaguzi kwenye uwanja wa ndege wakati wa kuwasili.

“Madaktari wetu hawakukaguliwa kama ilivyokawaida kwenye mifumo yetu na vyombo vya habari vya Comoro vilikuwa vinakuja kila siku kuwahoji madaktari wetu mmoja baada ya mwingine na ndiyo maana tunaona matunda ya wacomoro kutaka kuja kutibiwa Tanzania sababu ya kazi ya  Global Medicare,” alisema Mollel.


“Tutaendelea kuratibu kambi kama hizi bara la Afrika kutangaza fursa ambazo Tanzania tunazo na ambazo Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kwenye hospitali zetu kuanzia madaktari bingwa na vifaa vya matibabu vya kisasa kama CT Scan MRI,” alisema


Alisema kwa sasa tiba ni uchumi hivyo Global Medicare itaendelea kutangaza fursa zilizopo kwenye hospitali za Tanzania kupata wagonjwa wa nje ya nchi ambapo fedha za kigeni zitapatikana.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya daktari Seif Shekilage aliwapongeza madaktari walioshiriki kwenye kambi hiyo na kuahidi kuwa serikali itaweka mazingira mazuri kuhakikisha kambi kama hizo zinafanyika ili kuendelea kuifanya Tanzania kitovu cha utalii tiba.

4