Taasisi ya Lions Club imekabidhi vifaa tiba kwa Mbunge wa Jimbo la Kojani, Hamad Chande, kwa ajili ya vituo vya huduma za afya vilivyopo jimboni humo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao wa kusaidia maendeleo ya jamii.
Makabidhiano hayo yalifanyika Aprili 21, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti mstaafu wa Lions Club, Muntazir Bharwani, alisema taasisi hiyo ilipokea maombi kutoka kwa Mbunge huyo kuhusu uhitaji wa vifaa tiba. Kupitia michango ya wanachama wake, waliweza kununua na kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya.
Bharwani alieleza kuwa Lions Club itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaidia jamii kwa njia mbalimbali. Alibainisha kuwa mbali na vifaa tiba vilivyokabidhiwa, taasisi hiyo pia inapanga kuchimba kisima cha maji katika Kituo cha Afya Minungwi ili kusaidia huduma za afya na upatikanaji wa maji safi.
Aidha, Lions Club imekuwa mstari wa mbele kutoa misaada ya kijamii, ikiwemo chakula katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwenye maeneo mbalimbali kama vile mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, pamoja na kutoa huduma ya matibabu ya macho—yote yakifadhiliwa kupitia michango ya wanachama na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, aliishukuru Lions Club kwa moyo wa kujitolea na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo kwa kushiriki katika shughuli za kijamii.
“Taasisi kama Lions Club zina mchango mkubwa kwa jamii. Ni wakati sasa kwa taasisi zingine kuungana kwa pamoja katika kusaidia wananchi na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, hususan kwenye sekta ya afya,” alisema Chande.
Katika hafla hiyo, Naibu Waziri Chande alitangaza rasmi kujiunga na Lions Club ili kuendeleza ushirikiano wa kusaidia jamii. Aidha, alitoa wito kufunguliwa kwa ofisi ya taasisi hiyo visiwani Zanzibar kama ilivyo katika mikoa mingine ikiwemo Dar es Salaam.
Naye Asimuna Kipingu, ambaye pia alijiunga rasmi na Lions Club wakati wa hafla hiyo, alipongeza juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuifikia jamii kwa kushirikiana na serikali.
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na viti mwendo kwa ajili ya watu wenye ulemavu, magongo ya kutembelea, pamoja na mashine za kupima shinikizo la damu (presha).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED