Viungo wanne kubeba mikoba ya De Bruyne

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:28 PM Apr 22 2025
 Florian Wirtz
Picha: Mtandao
Florian Wirtz

JE, unawezaje kuziba nafasi ya kiungo mmoja bora zaidi katika historia ya Ligi Kuu England? Naam, hilo ndilo swali lisilopingika sasa linaloikabili Manchester City.

Kevin De Bruyne ataondoka kwenye Uwanja wa Etihad msimu huu utakapomalizika, baada ya miaka 10 ya kutoa huduma ya kipekee kwa klabu hiyo.

Mbelgiji huyo amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Kocha Pep Guardiola na kutawala soka la Uingereza.

Majeraha yamepunguza mchango wa De Bruyne katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Lakini hiyo ndiyo changamoto ambayo City na timu yao ya usajili inapaswa kuishinda wanapoanzisha enzi mpya. Kupata mbadala wake ni kama inaweza au  haiwezekani, lakini kuna safu ya vipaji vya kushangaza kote Ulaya ambayo huenda ikawasaidia kuziba pengo lake.

Hapa tunawaangalia viungo wanaoweza kuziba nafasi ya De Bruyne pale Manchester City:

#1. Florian Wirtz

Hakuna klabu duniani kote ambayo haiwezi kuboreshwa na uwepo wa Florian Wirtz. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, kupanda kwake kwa kiwango akiwa na Bayer Leverkusen kumekuwa kwa kushangaza na licha ya umri wake mdogo, tayari amejikusanyia mechi 200 akiwa na Die Werkself hao. 

Jeraha la msuli wa paja lilitishia kudhoofisha ukuaji wake wa mapema, lakini kiungo huyo mkabaji amerejea vyema.

Wirtz alihusika katika historia ya Leverkusen ya kutopoteza msimu uliopita, akifunga mabao 18 na kusaidia mabao 19 katika mashindano yote huku Kocha Xabi Alonso, akitengeneza timu inayomzunguka. 

Mtazamo wa kinda huyo wa kimataifa wa Ujerumani kwa kuonekana kutengeneza nafasi kunamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi barani Ulaya.

Haishangazi, uchezaji bora kama huu tayari umewavutia macho ya Manchester City, kati ya wengine wengi - na Wirtz bila shaka atakuwa kipaji cha kizazi chenye uwezo wa kuendeleza urithi wa De Bruyne. Ingawa si wachezaji wanaofanana kwa uchezaji.

Bei kubwa ya Wirtz - karibu zaidi ya pauni milioni 100 - ndio kitu pekee ambacho kinaweza kuwa tatizo katika kumnunua.

#2. Xavi Simons

Ukizungumzia vipaji vya thamani vya Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), anaingia Xavi Simons. 

Mholanzi huyo hatimaye alifanikiwa kuondoka kabisa katika klabu ya Paris Saint-Germain kipindi cha hivi karibuni cha usajili wa majira ya baridi huku akiendelea na maendeleo yake ya kuvutia akiwa na RB Leipzig.

Baada ya kufanikiwa kuchangia mabao 23 akiwa na kikosi hicho cha Ujerumani msimu uliopita, uvumi ulitanda juu ya mustakabali wa muda mrefu wa kiungo huyo, wakati Bayern Munich ikionyesha nia ya kumtaka msimu uliopita. 

Kusainiwa kwa mkataba wa kudumu na Leipzig hakujamaliza mazungumzo kama haya ya uhamisho kabla ya dirisha lijalo, na Ligi Kuu England imetajwa ni kivutio chake.

City watakuwa na kila sababu ya kumsajili Simons kama mrithi anayetarajiwa wa kiti cha ufalme cha De Bruyne. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye  hucheza kwa urahisi katika nafasi nyingi, ana kipaji cha asili, na ingawa yuko nyuma kidogo ya Wirtz na Jamal Musiala wa Bayern katika maendeleo yake, anga bado si kikomo kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi.

Mabao na pasi zake ni bora, pia anaweza kupatikana kwa bei nafuu ya takriban pauni milioni 60 msimu huu wa joto - mbadala wa bei nafuu zaidi kwa Wirtz.

#3. Morgan Rogers

Morgan Rogers alionyesha dalili za kuwa bora wakati wa nusu msimu wake wa kwanza akiwa Aston Villa, lakini amevuka matarajio yote wakati wa kampeni yake ya kwanza kamili huko West Midlands.

Uwezo wa kipekee wa Kocha Unai Emery, wa usimamizi umemfanya kiungo mkabaji, ambaye pia yuko vizuri nje ya boxi na pia kupata mechi zake za kwanza za Timu ya Taifa ya England na mchango wa mabao 20 katika mashindano yote msimu huu kwa ngazi ya klabu ni rekodi bora zaidi kwake.

Lakini City tayari walijua juu ya uwezo mkubwa wa Rogers kabla ya kutua kwake Villa. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alitumia miaka minne na kikosi cha Guardiola mwanzoni mwa maisha yake ya soka, ingawa alishindwa kuonekana kabla ya kwenda Middlesbrough mwaka 2023. 

Miezi sita baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Riverside, alikuwa ameonyesha vya kutosha kuwashawishi. Walilipa pauni milioni 15 kumsajili Rogers mnamo Januari 2024 na hajaangalia nyuma tangu wakati huo.

Rogers anaweza asiwe mbadala wa moja kwa moja wa De Bruyne, kwa sababu wawili hao ni watu tofauti sana na hawachezi nafasi sawa, ingawa nyota huyo wa Villa amedhihirisha uhodari wake chini ya Emery. Lakini kumekuwa na washambuliaji wachache wamefanya mengi mazuri zaidi msimu huu kuliko Rogers, ambaye ana kasi ya kufanya kazi bila kuchoka kuendana na ustadi wake wa ajabu na wa kiufundi.

#4. Morgan Gibbs-White

Rogers sio Mwingereza pekee anayeng'aa katika nafasi ya safu ya kati. Morgan Gibbs-White, anafurahia kampeni nyingine yenye mafanikio makubwa akiwa na Nottingham Forest, ambao wanatazamiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Wanaweza hata kushinda Kombe la FA iwapo wataifunga Manchester City katika nusu fainali.

Gibbs-White amekuwa muhimu kwa kampeni ya kustaajabisha ya Forest, hata kama hesabu ya wastani ya mabao matano na pasi saba si kubwa. 

Tofauti na Wirtz, Simons na Rogers, nyota huyo wa Forest ana uwezo wa kufanya kazi kama kiungo wa ulinzi zaidi katika kikosi kilichopangwa vizuri cha Kocha Nuno Espirito Santo.

Lakini Gibbs-White bado anajulikana kwa ubunifu wake wa kushambulia, kutafuta nafasi katikati ya mistari na kupiga pasi kwa mawinga. City walikuwa katika hali mbaya baada ya kupokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Forest mapema Machi huku De Bruyne akibadilishwa na Callum Hudson-Odoi.

Kwa mujibu wa gazeti la The Athletic, Gibbs-White ni mmoja wa wale wanaotathminiwa kama mbadala wa De Bruyne msimu huu wa joto - pamoja na Wirtz aliyetajwa hapo juu. Hakuna sababu ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kushindwa kuchanua zaidi chini ya Guardiola.