Sajili tano gumzo kabla msimu huu kumalizika

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:33 PM Apr 22 2025
Fei Toto
Picha: Mtandao
Fei Toto

WAKATI zimebaki raundi tatu tu kwa timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara kumaliza msimu, tayari baadhi ya klabu zimeanza kusaka wachezaji kwa ajili ya kuelekea msimu mpya, pamoja na mashindano ya kimataifa.

Baadhi ya viongozi wa klabu wamekiri wapo sokoni kwa sasa kusaka wachezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.

Hivi karibuni, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema msimu ujao watafanya usajili wa wachezaji kadhaa ambao si wengi sana kwa ajili ya kukiimarisha kikosi kilichopo ambacho kinaendelea kufanya vizuri.

Tayari kabla ya ligi kumalizika, zipo tetesi za klabu kadhaa za Tanzania kuingia mikataba ya wachezaji ambao inaona itawafaa.

Mwandishi wa makala haya anakuletea tetesi kadhaa za usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao.

1# Simba, Yanga vitani kumnasa Fei Toto

Imeelezwa Simba na Yanga hivi sasa zinapigana vikumbo kutaka kumsajili kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu akiwa na matajiri hao wa Chamazi msimu huu.

Pamoja na Azam imemwekea ofa, ikitaka aongeze mkataba, akiwa amebakisha mwaka mmoja, lakini haiondoi ukweli  hawezi kuhama kama vigogo hao wa soka nchini hawatapeleka dau nono linalohitajika.

Taarifa zinasema Simba ilipeleka ofa ya Sh. milioni 600, ikiwa ni ya kusaini mkataba,   ikitaka kumlipa Sh. milioni 400 kwa msimu wa kwanza na Sh. milioni 200, msimu wake wa pili.

Hata hivyo, chanzo kinasema, Yanga nayo imetia mguu, ilitaka kumrudisha nyumbani kwa kiasi cha Sh. milioni 750, ikimwahidi mshahara wa Sh. milioni 40 kwa mwezi.

Inadaiwa Yanga inapata kiburi kwa sababu itaingiza pesa ndefu kupitia mauzo ya kiungo wake mashambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, anayedaiwa ataondoka mwishoni mwa msimu kuelekea Wydad Casablanca ya Morocco.

2# Yanga kumrudisha Inonga Tanzania 

Usajili mwingine ambao umekuwa gumzo mitaani kabla hata ligi haijamalizika ni wa aliyekuwa beki wa Simba, Henock Inonga, anayedaiwa kutaka kurejea nchini, lakini safari hii atakuja kuvaa uzi wa njano na kijani.

Inonga, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), anadaiwa katika  mazungumzo na viongozi wa Yanga yaliyofikia pazuri ili kujiunga na timu hiyo msimu ujao.

Tabia ya Yanga kwa miaka ya hivi karibuni kusajili wachezaji wanaotoka Simba, au ambao walishawahi kuchezea timu hiyo kama, Jonas Mkude, Clatous Chama, Jean Baleke, Augustine Okra, kunawafanya mashabiki wengi nchini kuamini kwa asilimia nyingi beki hiyo wa kati  wa FAR Rabat ya Morocco, anaweza kutua Yanga bila matatizo yoyote.

3# Simba kusaka kiungo Benin

Klabu ya Simba imetaja inamfuatilia kwa karibu kiungo, Imourane Hassane, raia wa Benin, akiichezea pia timu ya taifa ya nchi hiyo kwa ajili ya kumwongeza katika kikosi chao cha msimu ujao.

Anakipiga kwenye Klabu ya Loto Popo ya nchini humo akitokea kwa mkopo Grasshoppers FC ya Ligi Kuu ya Uswizi.

Anatajwa moja kati ya viungo bora wa ukabaji wanaocheza Afrika kwa sasa ambapo anaangaliwa kama atafaa ili kuja kusaidiana na Yusuph Kagoma, ambaye ndiye tegemeo pekee kwa Kocha Fadlu David kwenye eneo hilo kwa sasa.

Fadlu, ameshawaambia mabosi wa Simba kusaka kiungo mkabaji kutoka nje, kwa kwenye nafasi hiyo anayeitendea haki ni Kagoma pekee, huku akimtaja kiungo, raia wa Nigeria, Augustine Okejepha kuwa aina yake ya uchezaji ni 'softi' sana kucheza namba hiyo.

4# Yanga, Azam vitani kumsajili kiungo Mkenya

Yanga ndiyo iliyoanza kuonyesha nia ya kumtaka kiungo mshambuliaji, Mohamed  Bajaber, aliyeonyesha kiwango cha hali ya juu akiwa na kikosi cha Harambee Stars katika kinyang'anyiro cha mechi ya kusaka tiketi ya kwenda kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani.

Hata hivyo, taarifa za hivi karibuni zinasema, Azam nao wametimba Kenya kuangalia uwezekano wa kuwapiku Yanga.

Bajaber alianza soka katika Academy ya Sherfield United iliyoko Mtaa wa Parklands, England kabla ya kufanyiwa majaribio na FC Midtylland ya Denmak mwaka 2021.

Mwaka wa 2022 Bajaber alijiunga na Nairobi City Stars ya Kenya na baadaye akatua kwa Maafande wa Polisi nchini humo Januari mwaka huu, timu ambayo anaichezea hadi sasa.

5# Simba kumsajili kinda Ngorongoro Heroes

Kwa sasa anafanya mazoezi ya kikosi cha Simba. Ameonekana mara kadhaa akiwa na kikosi hicho sehemu yoyote wanapokwenda kufanya mazoezi.

Huyu ni kiungo mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20, Morice Abraham.

Kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Klabu ya Spartak Subotica ya Serbia.

Taarifa zinasema Simba imempatia nafasi ya kufanya mazoezi ili kuthibitisha uwezo wake chini ya uangalizi wa Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Kinda huyo anacheza nafasi ya wingi ya kulia, kushoto na mshambuliaji msaidizi, yaani namba 10.