Baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Francis kilichotokea Jumatatu, Aprili 21, 2025, mjini Vatican, dunia imeingia kwenye kipindi cha majonzi, maombi na matarajio makubwa.
Papa Francis, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na kiharusi, alikuwa kiongozi anayependwa wa Kanisa Katoliki, akijulikana kwa unyenyekevu wake, juhudi za kuleta mageuzi ndani ya Kanisa, na msimamo wake wa kutetea haki za binadamu na mazingira.
Kwa mujibu wa Katiba ya Kitume, mazishi ya Papa yanapaswa kufanyika kati ya siku ya nne hadi ya sita baada ya kifo chake. Makardinali wanatarajiwa kukutana leo mjini Roma kuamua tarehe rasmi ya mazishi.
Wakati huo huo, dunia inasubiri kwa shauku kufahamu ni nani atakayechaguliwa kuwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki.
Makardinali kutoka pande zote za dunia wanakusanyika mjini Roma kwa ajili ya ‘Konklave’ – kikao cha siri cha kupiga kura kumpata Papa mpya.
Miongoni mwa majina yanayotajwa sana ni Kardinali Peter Turkson wa Ghana, mmoja wa viongozi waandamizi wa Kanisa ambaye kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki ya kijamii, mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kiuchumi duniani. Akiwa na umri wa miaka 76, Turkson anatajwa kuwa mmoja wa wagombea wakuu wanaopigiwa chapuo kumrithi Papa Francis.
Iwapo atachaguliwa, Kardinali Turkson atakuwa Papa wa kwanza Mwafrika katika historia ya kisasa, jambo ambalo litakuwa na maana kubwa si tu kwa Bara la Afrika bali kwa Kanisa zima, likiwa na zaidi ya waumini bilioni 1.3 duniani kote.
Kuchaguliwa kwa Papa kutoka Kusini mwa Ulimwengu – kama Afrika au Amerika Kusini – kunaweza kuwa ishara ya mwamko mpya katika Kanisa, unaoendana na uhalisia wa dunia ya leo ambapo idadi kubwa ya Wakatoliki inapatikana katika mataifa ya Kusini.
Majina mengine yanayotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Kardinali Matteo Zuppi wa Italia, anayeongoza juhudi za mazungumzo ya amani duniani, pamoja na Kardinali Luis Antonio Tagle wa Ufilipino, anayejulikana kwa ukaribu wake na vijana na uwezo wa kuwasiliana kwa lugha rahisi na ya kipekee.
Kwa sasa, macho na masikio ya waumini wa Kanisa Katoliki na jumuiya ya kimataifa yako mjini Roma, yakisubiri kwa subira tangazo rasmi kuhusu Papa mpya – kiongozi atakayekuwa dira ya kiroho, matumaini na mshikamano kwa ulimwengu wa leo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED