Dorothy Semu achukua fomu kugombea urais ACT Wazalendo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:49 PM Apr 22 2025
Dorothy Semu achukua fomu  kugombea urais ACT Wazalendo
Picha:Mpigapicha Wetu
Dorothy Semu achukua fomu kugombea urais ACT Wazalendo

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, leo Aprili 22, 2025, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Fomu hiyo imekabidhiwa kwake na Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi wa ACT Wazalendo, Shaweji Mketo, katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama zilizopo Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Dorothy Semu amesema hatua hiyo inaonesha dhamira yake ya dhati ya kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kisiasa kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.

"Nimechukua fomu hii kama ishara ya utayari wangu wa kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu wameshindwa kuendesha nchi na kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii," amesema Dorothy.

Aidha, ameeleza kuwa hatua yake ni sehemu ya harakati za kulinda demokrasia, haki za raia na thamani ya kura za Watanzania.

"Nimechukua fomu kama ishara ya utayari wangu wa kuongoza mapambano ya kulinda thamani ya kura na misingi ya demokrasia nchini," ameongeza.

Kwa mujibu wa Shangwe Ayo, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa chama hicho Dorothy atatoa dira na maono yake rasmi kupitia hotuba kwa Taifa ambayo ataitoa siku ya kurudisha fomu, ambapo tarehe ya tukio hilo itatangazwa hivi karibuni.

3