Ibada ya mazishi ya Papa Francis, itafanyika Jumamosi wiki hii ikiongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, katika Kanisa Kuu la Petro, jijini Vatican.
Taarifa ya Vatican leo imesema kuwa baada ya ibada hiyo, Papa Francis atazikwa siku hiyo katika Kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu, siku hiyo hiyo Aprili 26, 2025.
Tayari viongozi kadhaa wa nchi na serikali wamethibitisha ushiriki wao kwenye maziko hayo.
Vatican pia imesema kuanzia kesho Aprili 23, 2025 jeneza lenye mwili wa Papa litatolewa kwenye Kikanisa cha Nyumba ya Mtakatifu Marta Domus na kupelekwa kwenye Basilika ya kipapa ya Mtakatifu Petro, kama ilivyoelezwa katika kanuni ya maziko ya Papa wa Roma (Ordo Exsequiarum Romani Pontificis).
Imesema kabla ya uhamisho wa mwili huo, Mwadhama Kardinali Kevin Joseph Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu Katoliki la Roma, ataongoza misa.
Kwa mujibu wa Vatican, maandamano ya kuhamisha mwili yatapitia katika uwanja wa Mtakatifu Marta na uwanja wa Protomartiri Romani; kutokea kwenye Tao la kengele hadi kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro na kuingia kwenye Kanisa kuu la Vatican kupitia mlango wa kati.
Taarifa imefafanua kuwa katika madhabahu ya maungamo, Kardinali Camerlengo ataongoza ibada ya neno na mwisho na waamini wataanza kutoa heshima za mwisho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED