Kesi ya ukatili dhidi ya mtoto yahamishiwa mahakama ya wilaya

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:53 PM Apr 23 2025
Kesi ya ukatili dhidi ya mtoto yahamishiwa mahakama ya wilaya
Picha: Nipashe Digital
Kesi ya ukatili dhidi ya mtoto yahamishiwa mahakama ya wilaya

Kesi ya shambulio la kudhuru mwili inayomkabili Zaituni Mavula, anayedaiwa kumfanyia ukatili wa kipigo mtoto wa mdogo wake (jina tunalihifadhi), ambaye alikuwa akiishi naye jijini Dar es Salaam, sasa inahamishiwa kutoka Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kwenda Mahakama ya Wilaya.

Taarifa za kuhamishwa kwa kesi hiyo zimetolewa leo, Aprili 23, na Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda, katika viunga vya Mahakama ya Kinondoni, ambapo ameeleza kuwa ukubwa wa madhara aliyoyapata mtoto huyo unahitaji kesi hiyo kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya.

“Tumekwishaanza taratibu za kuhamishia kesi hiyo Mahakama ya Wilaya. Tumewasilisha maombi yetu na tunatarajia mchakato huo ukamilike ndani ya wiki mbili, japokuwa taratibu za kimahakama zinaweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja,” amesema Gloria.

Amesema uamuzi huo pia unalenga kuwezesha mawakili wa serikali kuweza kumtetea mtoto huyo ipasavyo, ikizingatiwa kuwa bado ni mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka 18.

Chanzo cha kesi hiyo kilitokana na taarifa zilizotolewa na raia wema kwa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Haki za Wanawake na Watoto (WAJIKI), kuhusu uwepo wa mtoto aliyekuwa akifanyiwa ukatili ndani ya nyumba ya Zaituni.

Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza, amesema baada ya kupokea taarifa hizo waliamua kufanya ufuatiliaji wa kina na hatimaye kuchukua hatua za kisheria kwa kumpeleka mtuhumiwa katika kituo cha polisi na baadaye kufungua kesi mahakamani.

Kwa sasa, mtoto huyo yuko chini ya uangalizi wa serikali ambapo anapatiwa matibabu na msaada wa kisaikolojia huku taratibu za kuhamisha kesi hiyo zikiendelea.