Ajira mpya 33,212 zamwagwa, Simbachawene agusia vijana wa NETO bungeni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:15 PM Apr 23 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

Rais Samia Suluhu Hassan jana ametoa kibali cha ajira kwa nafasi 33,212 za mwaka wa fedha unaoisha 2024/25 huku kada ya walimu ikipangiwa kupata nafasi 10,000 ambazo hazitafanyiwa usaili watachukuliwa kwenye Kanzidata.

Akihitimisha leo jioni hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Mwaka 2025/26 bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema “Katika kada ya walimu tutakwenda kwenye kanzidata tuendelee kupakua waliosalia ili kuhakikisha tunawamaliza, sio rahisi kuwamaliza maana waliofaulu wanaosubiri kupangiwa bado ni wengi.”

“Wamefanyiwa usaili na wapo tayari kufanya kazi na ndio maana walipokuja vijana wa NETO nikasema acha tuzungumze kusema kweli wana haki ya kusikilizwa na vijana wale walikuwa na mambo makubwa sana na mimi niliwaelewa, niseme kama tumejenga miundombinu ya elimu kwanini tusiongeze idadi ya walimu ili kukidhi mahitaji yanayotakiwa.”



“Nataka niwasemee vijana wa NETO maana huko wanasemwa sana na wenzao, wanasema tunasema uchumi wetu umekuwa sasa ni uchumi wa kati lakini tukisoma ripoti ya CAG tunaona kuna hela imepotea tunafikiri hii yote ingeangaliwa tungepata ajira sisi ya kuziba hili gap kwenda kufundisha wetu ambao ni watoto wanaohitaji elimu, sasa ukisikia hoja kama hiyo mzazi unasema mtoto huyu ni mkorofi? Mtoto anaomba kazi utasemaje mkorofi, sio mkorofi na kazi ya serikali ni kuendelea kutafuta fursa kuajiri kwa mahitaji ya serikali.”