Wasira: Viongozi wa dini wametutia moyo kuendelea na uchaguzi mkuu

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:30 PM Apr 23 2025
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,  Stephen Wasira.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini kwa ushauri kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kubariki uchaguzi huo uendelee huku, ikisisitiza kuwa haidharau maoni yanayotolewa.

CCM imesisitiza kuwa haipuuzi ushauri mbalimbali unaotolewa kuelekea uchaguzi huo, lakini imesisitiza hautaahirishwa kwa kuwa mageuzi na mabadiliko ni jambo endelevu na haiwezi kuwa hoja ya kuahirisha uchaguzi.

Hayo yameelezwa leo Chamwino mkoani Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,  Stephen Wasira, alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

"Uchaguzi utaendelea sio kwamba tunapuuza mawazo, tutaendelea kuzungumza mambo ambayo yanaendelea, na tunashukuru sana nchi imetulia. Viongozi wetu wa kiroho wametuongoza wametupa ushauri mzuri sana na mimi nashukuru sana kwa kututia moyo na kutuambia uchaguzi uendelee lakini kwa amani," amesema Wasira.

1

Wasira amesisitiza kuwa CCM ni chama kinachozungumza na kuhimiza amani ndio maana taifa limekuwa na utulivu kwa miaka 60, na kwamba hilo linafanya chama kijivunie kwa kuwa ni ushahidi kwamba kinaweza kusimamia amani.

Pia amesisitiza kuwa haki iko ndani ya amani na kwamba ukiondoa amani utavunja haki za watu wengi hususan wanyonge, "ukiondoa amani watakaoumia hasa ni wanawake, watoto na walemavu."

"Amani ni lazima sasa kuna wanaosema haki, na sisi tunasema ndani ya amani kuna haki, na haki hiyo inalindwa na amani kwa sababu ukiiondoa watu wengi wataathirika wala sio mtu mmoja ni wengi sana na ushahidi wake upo, sisi tumepokea wakimbizi maelfu kutokana na kuvunjia kwa amani kwa majirani zetu," amesisitiza Wasira.
2