CWT Pwani watakiwa kuweka mikakati kuimarisha maadili shuleni

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:25 PM Apr 23 2025
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala.

Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Pwani wametakiwa kuandaa mikakati madhubuti ya kuhakikisha maadili ya wanafunzi mashuleni yanaimarika kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Wito huo umetolewa leo Aprili 23 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa CWT Mkoa wa Pwani uliofanyika mjini Kibaha.

Akizungumza katika mkutano huo, Twamala amewataka walimu kuangalia kwa kina mwenendo wa maadili ya wanafunzi wanaowafundisha, na kutoa ushauri stahiki katika shule zao ili kusaidia kuwajenga watoto wenye maadili mema.

“Tujitafakari kuhusu maadili ya watoto tunaowalea. Ni wajibu wetu kushauri ndani ya shule zetu ili watoto wetu wakue katika misingi mizuri ya maadili, kwani kwa sasa hali si ya kuridhisha,” amesema Twamala.

Katika mkutano huo ambao ulihusisha pia uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kwa ngazi ya mkoa, Twamala ametoa wito kwa wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa, uwajibikaji na maono ya kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha.

Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha, akiwasilisha risala ya chama, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi ya walimu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Hata hivyo, Shesha ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili walimu, ikiwemo malimbikizo ya madeni ambayo bado hayajalipwa tangu mwaka 2017, licha ya kupitia hatua za uhakiki. Madeni hayo yanahusisha fedha za uhamisho, likizo, na nauli.

Ameongeza kuwa bado kuna walimu ambao hawajapandishwa madaraja licha ya kuwa wanakidhi vigezo. Pia ameeleza kuwa changamoto nyingine ni kutotekelezwa kwa mabaraza ya wafanyakazi na uhaba wa walimu wa shule za msingi na sekondari katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.

Mkutano Mkuu wa CWT Mkoa wa Pwani umefanyika kufuatia mikutano ya ngazi ya wilaya ambayo nayo iliambatana na uchaguzi wa viongozi katika maeneo husika.

Meza Kuu.