SHIRIKA la Umoja wa Mataifa (UN) na wadau wa mazingira wametoa wito kwa jamii kuongeza juhudi, ili kudhibiti uchafuzi wa plastiki na kulinda mifumo ya ikolojia ya baharini.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika leo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwakilishi Mkazi wa UN nchini, Susan Namondo, alisema kaulimbiu za mwaka huu za siku ya mazingira na bahari zinaonyesha uongozi unaozidi kukua katika usimamizi wa mazingira.
“Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, ‘Kumaliza uchafu wa Plastiki’, na ya Siku ya Bahari Duniani, ‘Uvuvi Endelevu Unamaana Zaidi’, zinaonesha wajibu wetu wa haraka kuchukua hatua kwa pamoja kulinda binadamu na sayari,” alisema.
Namondo alisema kuwa zaidi ya tani milioni 11 za plastiki huingia baharini kila mwaka idadi ambayo inatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2040 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Alisema pia kwa sasa inakadiriwa kuwa kati ya tani milioni 75 hadi 199 za plastiki zimeshaingia na kuchafua bahari na zaidi ya spishi 800 za baharini zimeathirika kwa kula plastiki, kufungwa na taka, na kupoteza makazi yao hali inayohitaji ushirikiano wa haraka na wa kimataifa.
“Uchafuzi wa plastiki siyo tu suala la mazingira ni suala la kibinadamu, unawaathiri zaidi watu waishio pwani, hasa wanawake na wavuvi wadogo ambao maisha yao hutegemea mifumo ya ikolojia ya baharini yenye afya.”
Alisema Tanzania ikiwa na zaidi ya kilomita 1,400 za pwani ya Bahari ya Hindi, ina nafasi nzuri ya kuongoza juhudi za uhifadhi wa bahari. Aidha, alisema kama mifumo ya ikolojia ya ya pwani ikiwemo mikoko, miamba ya matumbawe, na maeneo ya majani baharini ikitunzwa ni muhimu kwa bayoanuwai ya baharini, utalii, uvuvi, na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika tukio hilo hilo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) nchini, Clara Makenya, alisema suluhisho la uchafuzi wa plastiki ni zaidi ya kampeni za usafi.
Alisema pia kuna umuhimu wa ushirikiano wa sekta mbalimbali na katika kuzuia taka za plastiki kuingia kwenye mazingira. Makenya alisema kwa upande wap wanachukua hatua jumuishi kwa ngazi zote za jamii ili kuhakikisha suala la uchafu wa plastiki linatokomezwa.
“Hatua hizo zitawakilisha na kutetea kila ngazi kutoka kwa washirika wa utekelezaji wa sheria, hadi kwa wajasiriamali wanaoonesha ubunifu wa kuchakata plastiki, na bila kusahau shughuli za usafi zinazoongozwa na jamii,” aliongeza.
Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Jamal Baruti, alisema kuwa kwa sasa baraza hilo linafanya utafiti kuchunguza kiwango cha uchafuzi wa plastiki katika vyanzo vya maji nchini.
Maadhimisho haya yanakuja wakati muhimu, ambapo jumuiya ya kimataifa inajiandaa kwa ajili ya Mkutano wa tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari, unaotarajiwa kufanyika Juni 9 hadi 13 huko Nice, Ufaransa. Mkutano huo unalenga kuharakisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14: Maisha chini ya Maji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED