Wazazi wa watoto pacha wamomba Rais Samia msaada wa Bima ya Afya

By Hellen Mwango , Nipashe
Published at 07:31 PM Jun 05 2025
Wazazi wa watoto pacha wamomba  Rais Samia msaada wa Bima ya Afya
Picha:Mpigapicha Wetu
Wazazi wa watoto pacha wamomba Rais Samia msaada wa Bima ya Afya

Wakazi wa Mbagala Kingugi, Wilaya ya Temeke Mbwanyi Shabani (35) na mke wake Amina Bakari wanamuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kuwasaidia kwa hali na mali ili watoto wao mapasha watatu walipiwe huduma ya bima ya afya na lishe bora ili kuwanusuru na maradhi yanayowakabili ikiwamo utapiamlo.

Wakizungumza na Nipashe nyumbani kwao Kingugi kwa nyakati tofauti, Bakati alisema watoto wake kwa sasa wanahitaji msaada mkubwa kwa kuwa maisha yao yako hatarini ikiwamo mmoja vipimo kuonesha kuwa na moyo mkubwa.

Alisema hawana uwezo wa kuwapeleka hospitali kila wakati kutokana na hali duni waliyonayo na kwamba mume wake anatembeza viatu mkononi ikitokea akapata wateja watapata chakula na haikidhi hata kununua pampasi.

“Namuomba Rais Samia yeye ni mama anisaidie watoto wangu wapate huduma ya bima ya afya wanazidi kudhoofika kwa maradhi, hawapati lishe bora, hawana mavazi nawaomba na Watanzania wenzangu mnisaidie chochote mtakachojaaliwa napokea ili watoto wangu wapate warejee katika ukuaji bora.

“Wana miaka miwili na miezi mitatu lakini mpaka sasa wanashindwa kutembea kutokana na kukosa lishe bora na mlo kamili, wakati mwingine wakizidiwa na maradhi nashindwa kuwapeleka hospitali sina uwezo wa kifedha kwa ujumla,” alisema Amina.

Akizungumzia kuhusu msaada wa serikali katika kata yao alisema walipokelewa na Ofisa ustawi wa Kata ya Kingugi, Monica Kapufi walipokea msaada wa lishe bora na chakula mara moja, lakini kilipoisha aliwataka kuwa na subira mpaka atakapopatikana msamaria mwema.

“Hali ya watoto kama unavyiona mmoja tu hana shida hawa wawili wanasumbuliwa na maradhi yanayohitaji huduma za matibabu mara kwa mara(Nipashe ikiwa eneo la tukio iliwaona watoto muda wote wakilia njaa baada ya kupatiwa chakula walitulia), ninaomba wenye nguo, chakula fedha maana tunaishi chumba cha kupanga tunahitaji msaada mkubwa sana kuokoa maisha ya watoto wangu,” alisema Amina huku akibubujikwa machozi.

Kwa upande wake baba wa watoto hao, Shabani alisema anafanyabiashara ya kuuza viatu kutembeza mkononi kama machinga na kwamba watoto wake walizaliwa njiti huku mmoja akiwa amezaliwa kwa njia ya kawaida na wawili kwa njia upasuaji.

Alisema kutokana na kipato chake duni anashindwa kumudu kuwahudumia watoto wake ikiwamo huduma ya afya, mlo kamili, lishe bora na mavazi.

“Namuomba Rais Samia na Watanzania wenzangu wanisaidie kunikatia bima ya afya kwa ajili ya watoto wangu, wawili wanasumbuliwa na maradhi ikiwamo ya moyo mkubwa, sina kipato cha kumudu kumpatia matibabu stahiki, wana utapia mlo kwa kukosa lishe bora.

“Ninawaomba watanzania wenzangu wenye mapenzi mema kunisaidia watoto wangu ni wa kike,wakati mwingine nikitembeza biashara sipati wateja watoto wanakosa mlo hata ule mmoja naomba msaada wenu Watanzania wenzangu,” alisema shabani huku akibubujikwa machazi.

Alisema yeyote mwenye mapenzi mema awasiliane nao kwasimu yake ya mkononi ya Airtel 0697047943 yenye majina ya usajili ya Mbwanyi Shabani.