Waziri Mchengerwa ashuhudia utiaji Saini mikataba miradi ya maji

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:10 PM May 07 2025
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za familia na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mohamed Mchengerwa
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za familia na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mohamed Mchengerwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za familia na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mohamed Mchengerwa, ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya Maji itakayojengwa katika Vijiji vitatu vya Mloka, Mbunju Mvuleni pamoja na Ndundutawa Wilaya ya Rufiji.

Miradi hiyo ya maji itakapokanilika itahudumia Wananchi 16, 593 na kusaidia kupunguza kero ya Maji katika maeneo hayo.

Hafla ya Utiaji Saini wa Mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo imefanyika katika Kijiji Cha Mloka Kata ya Mwaseni  Mei 6, 2025.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Rufiji Mhandisi Alkam Sabuni, amesema ujenzi wa Miradi ya Maji katika vijiji hivyo utagaharimu kiiasi cha Shilingi 791,068,682.56.

"Katika Kipindi cha mwezi Juni 2025 hadi Oktoba 2025 Wananchi wapatao 16,593 wa vijiji vitatu vya Mloka, Mbunju Mvuleni na Ndundutawa wanaenda kunufaika na huduma ya Maji safi na salama na yenye kutosheleza, ambapo miradi hii itakapokamilika itaongeza hali ya upatikanaji wa Maji kutoka asilimia 86.6 ya sasa hadi asilimia 97.3" amesema.

Sabuni ameongeza kuwa RUWASA Wilayani Rufiji inatoa huduma katika Vijiji 38 vyenye Jumla ya Watu 157,412 kwa Mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Kwa upande wake Waziri Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji amesema uwepo wa miradi hiyo  itakapokamilika kupunguza adha ya Wananchi kwenda kuchoma Maji katika Mto Rufiji.

"leo tumeandika historia katika changamoto ambazo tumekuwa tukizipata kwa muda mrefu leo tumezimaliza na matarajio yangu kwamba Mkandarasi sasa ataanza kazi mara Moja" amesema Mchengerwa.