DORIS LUVANDA; Kibarua mtoto shambani na stendi, hadi mwekezaji aliyeajiri watu 100

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:30 PM Apr 18 2025
Doris Luvanda, akiwa kazini
Picha: Christina Mwakangale
Doris Luvanda, akiwa kazini

UYOLE, ni sehemu maarufu mkoani Mbeya, pakiwa njia panda inayowakaribisha wageni wanaoingia jijini Mbeya wakitoka Iringa na Dar es Salaam.

Pia, ndiko kwenye njia panda ya barabara ziendazo na kutoka Malawi, pia Zambia. 

Vilevile, panabaki ndiko kituo cha kuaga jiji la Mbeya, kwa safari ya Barabara Kuu kuisaka wilaya ya Mbarali, pakiwa na wasifu wa kimazingira kwa kifupi  pako bize kwa biashara hasa za barabarani.

Hapo ndiko penye mzizi wa makuzi yake mwanamama Doris Luvanda (47), ambaye ana tafsiri yake kimaisha katika kumbukumbu yake; magumu aliyopitia maishani yasiyosahaulika.

Pia, upande wa pili ina zawadi kuwa eneo lililomtoa kimaisha, akianzia kuuza chai barabarani, leo hii ni mfanyabiashara maarufu anayeajiri zaidi ya watu 100.

Hapo ndipo Nipashe, ikamgongea hodi kutaka kupata maelezo ya kina.

Mara moja mazungumzo hayo yakadhihirisha hulka ya ujasiri, kujiamini na yu mtu wa watu katika mambo yake.

Pia, hakuficha wajihi wake kwamba yu mpambanaji anayechukia umasikini, akapambania hilo kuwainua wadogo zake hadi wanawe, mmoja mzaliwa tangu mama huyo akiwa kijana wa miaka 16.

HATUA ZAKE ZILIVYO 

Doris Simon Luvanda (47), ni mzaliwa wa pili kwenye familia ya watoto watano, kati yao wa kike wanne na mmoja wa kiume. 

Anasema, amezaliwa wilayani Mufindi eneo la Kibaoni, mkoa wa Iringa.  

Wazazi wake mwaka 1988 waliamua kuhamishia makazi yao na kuanza maisha Uyole, mkoani Mbeya.

“Sisi tukiwa wadogo mwaka 1990 wakatuchukua kuhamia Uyole, nikasoma Shule ya Msingi Sanga, Uyole Mizani. Bahati mbaya wazazi wangu wakaishi muda mfupi sana Uyole.

“Mama akaanza kuumwa, akaumwa magonjwa yasiyotibika, akafariki! 

Lakini baba na mama wakapishana muda mfupi. Baba naye akafariki na ndio safari yangu ya mapambano nikiwa na umri mdogo ikaanza,” anasimulia.

Mama Doris akaendeleza simulizi kuwa: “Nimezaliwa mwaka 1978, baba yangu amefariki mwaka 1996 na mama 1994 hata miaka 20 nilikuwa sijafikisha. Mama anavyofariki 1994 nilikuwa na miaka 16.”

Anasema, baada ya mama yake kufariki baba akawaacha, akirejea kwao wilayani Mufindi.

“Baba alikuwa na wake wengi. Mama alipofariki baba akarudi kijijini, akatuacha sisi Uyole, akasema turudi kijijini tukakataa tukabaki Uyole! wote watoto watupu mimi ndio mkubwa.

“Dada yangu wa kwanza alikuwa yupo Zambia, ameenda kuhangaika na maisha... nina miaka 16 basi nikaanza maisha ya mapambano.”

VIBARUA SHAMBANI

Doris anasimulia, hangaiko lake likaanzia kufanya vibarua kwenye mashamba ya Shirika la Kilimo Uyole na ya watu binafsi.

“Nilifanya vibarua kwenye mashamba ya watu ambako wanangoa maharage unaenda unafanya vibarua. Siku nyingine vibarua vinakuwa hamna unalala na njaa. Tumelala sana njaa, tumelala giza, tumekosa viatu, tumekosa nguo.

“Yaani ulikuwa ni msoto wa muda mrefu. Mwaka huo unapopalilia mahindi unalipwa Sh. 700 au 500 na huo mstari wa mahindi kupalilia, dada (mwandishi), sitamani kukumbuka!

“Hiyo pesa utanunua kisado (kidumu) cha mahindi na ukasage, ubakize hata 100 utunze akiba. Mboga tunachuma mashambani zilizojiotea tu, tukifika tunachemsha tunakula tunalala.

“Unaanzia Uyole pale kuanzia kwenye miti ya kilimo (Shirika la Kilimo Uyole) mpaka kwenye ile barabara ya treni (daraja la treni), tunapalilia na mdogo wangu huo mstari.

“Mstari mmoja tunapalilia siku mbili, kwa sababu ni wadogo na ule mstari ni mrefu mnoo! Kwa hiyo, tulikuwa tunachukua mstari mmoja tunapalilia na mdogo wangu,” anasimulia Doris.

Anaitafsiri kwake ilikuwa kama giza maishani, akisema hakuacha kuhangaika huku na kule pamoja na wadogo zake, alikuwa haelewi.

“Mbele giza, nyuma giza, na kushoto giza, kulia giza, hatumuoni ndugu wakati mama yupo ndugu walikuwapo wengi, ghafla tulijikuta tupo jangwani.

“Tupo peke yetu, hatuna mtu hakuna anaetutazama wala kutuhurumia, kwa hiyo mimi hiyo ikawa inaniongezea kujiongeza maana mimi ndio mkubwa,” anaeleza.

Doris anasema kutokana na hali ya kiuchumi waliyokuwa nayo, hakuweza kuendelea kusoma, pale alipomaliza elimu ya msingi katika shule ya Sanga mwaka 1992.
Baadaye mwaka 1996, anasema akiwa matesoni, akajitokeza mtu aliyemdokeza aanze maisha mapya, pengine angefanikiwa.

Anasimulia: “Akanifuata mtu mmoja akaniambia kuna mwanaume anataka kukuoa ana uwezo, akawa ananielekeza kwamba huyo mtu yupo Njombe (sasa mkoa).

“Kwamba mwanaume ni tajiri ana maduka atakulea na watoto (wadogo zake). Nikawa nimejaribu kukataa, lakini maisha yakazidi kuwa magumu.

“Basi nilikuwa na rafiki yangu mmoja tukashauriana, akasema nenda kaishi naye, unaweza ukawakomboa watoto...

“Kweli nikabebwa kama kifurushi nikapelekwa huko Njombe, nikaenda kuanzisha maisha na huyo mwanaume, ila nilipoanzisha maisha na yule mwanaume nikagundua nimeingia kwenye matatizo.

“Yule mwanaume kumbe ana wanawake wengi, mimi nilikuwa mwanamke wa 10. Mimi kipindi hicho hata miaka 18 sijafika, alikuwa (mwanaume) ana miaka 30 na zaidi. Ni mtu mzima nakuja kugundua tayari nilishakwenda huko, nikasema hapa ngoja niondoke.”

KUREJEA NYUMBANI

Doris anasema, alipoona maisha ya kuolewa magumu, hata mwaka mmoja haukuisha, akaamua kurudi Uyole.

“Narudi nyumbani, kumbe mimi tayari ni mjamzito, yaani matatizo ndio yakazidi kuwa magumu. Hapo ni kulala na njaa na ujauzito, mambo hayaendi basi baadae Mungu akanisaidia kwenye vibarua...” anaeleza.

Kwa mujibu wa mama huyo, hata hatua yake ya kujifungua katika Hospitali ya Wazazi ya Meta jijini Mbeya, ilikuwa kwa msaada wa majirani wa Uyole.

AJIPANGA BAADA KUJIFUNGUA

Mama huyo anasema, baada ya kupata nguvu kutoka kujifungua, alipata wazo kuanzisha biashara ya kuuza chai na maziwa eneo la Njiapanda Uyole.
“Nikawa naenda kuuza chai Stendi ya Dar es Salaam pale Uyole. Kuna stendi inaitwa ya Dar es Salaam mahali wanapopandia watu magari wanaotoka Mbeya, ni maarufu sana!

“Pia, ipo stendi ya Usangu hapo hapo, nikaanza kuuza chai, chupa moja ya rangi na ya nyingine maziwa. Napika na makande. Mungu anasaidia, mambo yanaenda nacheza michezo (upatu).

“Mara nikaongeza idadi ya chupa, zikawa mbili mara tano, kumi, ishirini. Nambeba na mtoto na wafanyakazi ni wadogo zangu, basi nikakuta mambo yanaenda, nauza naweka hela!  Chai nilikuwa nauza shilingi. 30,000 hadi 100, 000,” anaieleza Nipashe.

Doris anasimulia mpangilio wao wa kazi, ratiba waliipanga baadhi ya wadogo zake kuwa naye kibaruani na mmoja anabaki nyumbani kusukuma chapati.

“Nikawa naiona biashara ya catering (mapishi) nikatamani kupika vyakula vya masherehe, nikawa nanunua vyombo natunza ndani. Baadae nikaanza kufanya matangazo,” anaeleza.

Anadokeza kwamba hakuwahi kufanya upishi mkubwa, alikosa mbinu za kujifunza, ingawa alipenda kupika akiwa na umri mdogo, kila alichoona anakatamani kujifunza kilivyopikwa.

“Nikatafuta wapishi wanaopika Mbeya wale maarufu, nikaenda kuomba kibarua, kumbe najifunza nijue kuku wanakataje, viazi wanakataje, hiki wanapikaje?

NURU YAJITOKEZA

“Nikawa najifunza nilivyoona nimefikia level (hatua) ambayo naweza kupata oda ya watu 25 nashukuru Mungu.

“Nilipika kile chakula kilitoka vizuri, kilikuwa chenye ubora, wakasema hatujawahi kula chakula kizuri kama hiki.

“Sasa, tuna sherehe ya watu wengi watu 100 utatupikia mwezi ujao! Kweli nikapika, ikatoka bomba na wakati huo ilitakiwa kila kitu nipike nilikuwa sina wapishi wengine wanaojua kupika.

“Napika mwenyewe vyote, watakochonisaidia ni kumenya nyanya kuchambua mboga, lakini kupika ni lazima nipike mimi nikaanza kupata oda watu 400,” anasimulia

AANZA KUTOKA

Doris anasema, wakati  akiendelea na biashara ya kupika, akafanikiwa kuweka akiba ya fedha hadi kupata makazi yake rasmi ya kufanyia biashara hapo.

“Nikanunua nyumba kubwa yenye vyumba 13, maana nilikuwa napikia kwenye nyumba za watu za kupanga, kwa hiyo kuuza stendi sikuacha, nikaendelea kuuza,” anaeleza. 

ALIVYOFIKIA NDOTO

Kwake Doris, ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa mpishi mkubwa, sasa amefanikiwa akimiliki majiko tofauti, wilayani Mbarali na Chunya.

“Ndoto yangu kubwa ilikuwa nije kuwa mpishi mkubwa, mpishi bora Nyanda za Juu Kusini au wapozungumzia Tanzania, nilitamani siku moja na mimi jina langu litajwe. Kweli sasa Malkia wa Nguvu Nyanda za Juu Kusini, Mpishi Bora wa Chakula.

“Nilikuwa natamani sana na tangu nikiwa mtoto ambaye hata kwenye yale maisha ya kufanya vibarua, sikuwahi kuamini kama nitakufa maskini, yaani hilo ndio namshukuru Mungu.

“Nikifanya kitu kizuri, nasema na mimi nitakuja kununua hiki, nitakuja kufanya, yaani mtu mwingine ananichukulia kama nina tatizo la akili.

“Lakini nilikuwa namaanisha kweli, nikapata nyumba watu wengi walishangaa, nikawa na kampuni, nikanunua gari aina ya Coaster, nikawa nabebea na chakula...niliagiza Japan, ikaja kwa majina yangu.

“Wakazi wa Mbeya, walishangaa Coaster nilinunua milioni 48, iliingia mwaka 2017 mwezi wa saba. Nikaendelea, baadae nikaanza kujishughulisha na biashara za majiko, nikaacha kutembeza chai nikaanza kufanya biashara.

“Kuna baa moja Uyole ilikuwa maarufu ilikuwa inaitwa Makasini. Wakanipa upande wa chakula, nikauza pale miaka saba, baadae nikatoka pale nikawa nimekua. 

“Nilipoenda Makasini nikaanza kuuza Sh. 300,000, Sh. 500,000 hata Sh. 700,000. Nikaenda Mbeya Pazuri nikashangaa nauza shilingi milioni mbili mpaka tatu, nikamshukuru Mungu. Hayo ni mauzo ya siku moja! Nikafungua tawi Mbalizi, Tughimbe lakini hapakufanya vizuri.

“Sasa nauza chakula Chunya Pazuri na Mbarali Pazuri. Pia, mimi ni mchimbaji, nachimba madini aina ya dhahabu Chunya huko Ifumbo.

“Biashara ya 'catering' imekuwa, kwa sababu napika chakula, yaani napika chakula naweza kusambaza chakula Iringa na Mbeya, Songwe.

“Napika chakula Mbeya na wilaya zake zote, naweza kutoa huduma ya chakula Kyela, yaani kila sehemu tumekuwa na vyombo vingi tuna usafiri tuna wapishi wabobevu.

“Sisi popote kambi, mtu akiwa na msiba au sherehe. Mkusanyiko wa aina yoyote ule tunaondoka tunakuja tunalisha maelfu,” anaeleza katika lugha ya kujigamba kibiashara 

AAJIRI KIKUNDI

Doris anasema, kazi hiyo imemfanya kuajiri kikundi, wamo wanawe waliomaliza elimu ya sekondari wakajiunga naye kwenye biashara.

“Watu wanasomesha, watu wanajenga, watu wanaishi kupitia mimi. Ninao watu ambao ninafanya nao kazi kutoka ninaanza harakati zangu, niko nao sambamba.

“Wapo waajiriwa wapya ambao tumeendelea kuwapata wanakuja wanafanya kwenye catering wanafanya kwenye jiko langu la Mbarali, wanafanya kwenye jiko langu la Chunya, pia wapo wafanyakazi nikihesabu ni karibu wafanyakazi 100,” anaeleza.

AHAMASISHA KWA UCHUNGU

Doris kupitia kurasa za kijamii mtandaoni. anasema anazitumia kuhamasisha wanawake wenzake, kufanya shughuli za kujikwamua kiuchumi. 

Anaiambia Nipashe kuwa: “Nimekuwa mwanamke ninayehamasisha sana kufanya kazi, kwa sababu ninauchukia umasikini kupita kawaida. 

“Kwa sababu zipo shida niliwahi kupitia mimi nazaa mtoto wangu yule wa kwanza, nilikosa nauli ya kuendea hospitali. Naumwa uchungu nikiwa Mbeya Uyole, maana kwa yule mwanaume nilitoroka” anasema.

SAKATA LA UCHUNGU

“Ndio narudi nyumbani, nakuja kugundua ni mjamzito, nikaendelea kulea ile mimba nalea kwa vibarua siku naumwa uchungu sina pesa.

“Uchungu ulinianza saa tano usiku nikafika nao mpaka asubuhi, nikatembea kama kilomita moja na nusu, kwenda kwa mkunga anizalishe mkunga akasema huwa sizalishi uzazi wa kwanza.

“Ikabidi nirudi nyumbani nimefika nyumbani, rafiki yangu mmoja akaja anaitwa Amida Sanga, mkazi wa Dar es Salaam akaniambia “mbona nimekuotea ndoto kama unaumwa?”

“Nikamwambia naumwa uchungu tangu jana usiku, akasema twende hospitali, nikamwambia sina hata mia, akatoka akaenda akahangaika huko akaja kunichukua alivyonichukua akanipeleka Hospitali ya Wazazi Meta (jijjini Mbeya).

“Usiku nikajifungua miaka hiyo kujifungulia Meta ilikuwa ni Sh. 3,000 mwaka 1997, huwezi amini hela ya kutokea hospitali sikuwa nayo.

“Nililala siku mbili nimesharuhusiwa, lakini nilikaa siku mbili Sh. 3,000 hamna, akaja rafiki yake mama anaitwa Mama Huruma wa Uyole na Mama Sam, akanilipia ile Sh. 3,000 siku ya tatu.

“Wakanilipia wakanisagia unga wakanipa na hela ya siku mbili, huyu ni mtoto wangu wa kwanza wa kike jina anaitwa... maisha magumu kuliko magumu niliyowahi kuishi.

“Fikiria mwanamke aliyetoka kujifungua, njaa ya mtu aliyejifungua na mtoto ananyonya maziwa halafu kula kutoka juzi hajala, siwezi kutembea, hakuna simu kwamba utampigia mtu simu.

“Niliteseka dada (mwandishi) nikasema sijui nitupe mtoto na mimi nijiue? Yaani maisha, njaa inauma yaani sijui nikuelezaje? Maziwa hayamo.

Anahitimisha kumbukumbu hapo kwa kauli: “Ninauchukia umaskini, inaniuma na ndio maana nimekuwa nikihamasisha watu tokeni mwende mkapambane.

“Tutengeneze msingi watoto wote wasije wakaishi maisha tuliyoishi, ndio maana nilijitolea kuhamasisha watu kufanya kazi.

*IJUMAA IJAYO USIKOSE SIMULIZI YA UYOLE