Ijue PID; ugonjwa unaomtesa mama, lakini wanaouelewa vilivyo wachache

By Mary Mbikiwa , Nipashe
Published at 10:17 AM Oct 17 2024
Ijue PID; ugonjwa unaomtesa mama, lakini wanaouelewa vilivyo wachache
Picha: Mtandao
Ijue PID; ugonjwa unaomtesa mama, lakini wanaouelewa vilivyo wachache

INAPOTAJWA ‘Pelvic Inflammatory Disease’ au kifupi PID, taafsiri yake katika lugha rahisi ni ugonjwa wa maambukizi ya vimelea kwenye viungo vya mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Hapo, viungo vinavyoathiriwa zaidi ni shingo ya kizazi, mirija ya uzazi, tumbo la uzazi (uterasi) na mifuko ya mayai aliyo nayo mwanamama. 

Ugonjwa wa PID unatajwa kuwapata wanawake wenye umri wowote, lakini kwa kiwango kikubwa wenye umri kati ya miaka 20 mpaka 40 ndio wanaoathiriwa zaidi. 

Sababu kuu ya ugonjwa huo kuendelea kuwasumbua wanawake wengi, ni pamoja na kufanya ngono isiyo salama au kujamiiana bila ya kutumia kinga, maarufu kitaalamu ‘ngono zembe’. 

Ugonjwa huo kwa kawaida husababishwa na maambukizi ya vimelea na wapo wa aina nyingi wanaosababisha shida hiyo ya PID na mara nyingi inakuwa na uwiano wa kawaida wa vimelea kwenye uke unakuwa umevurugika, hivyo kuruhusu vimelea hatari kuzaliana. 

Wanawake ambao wamewahi kuugua kisonono, klamidia, au magonjwa ya zinaa, wanatajwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huo. 

Mambo mengine ambayo yanaweza kuongeza hatari ya PID ni pamoja na kufanya ngono kabla ya umri wa miaka 18, kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, pia kufanya mapenzi bila kutumia kinga.

 Hata vivyo, kuna viashiria vya ugonjwa huo, kwa baadhi ya wanawake wenye ugonjwa wa PID wanaweza wasionyeshe dalili zozote, huku wengine ambao wanasumbuliwa na 

ugonjwa huo, wanaweza kuonyesha dalili zifuatazo:  

Kuna maumivu kwenye tumbo chini ya kitovu; kutokwa na uchafu mweupe mzito sehemu ya siri kwa mwanamke, ikiwa na rangi ya maziwa mtindi; wengine hutokwa na uchafu wa rangi ya njano; pia, wapo wanaotokwa na uchafu wenye harufu ya shombo la samaki. 

Hata hivyo, baadhi yao huhisi maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu ya nyonga, kutokwa na damu ya ‘mabonge mabonge’ wakati wa hedhi, kutokwa na majimaji mengi ukeni yenye harufu 

mbaya; kuvurugika kwa siku za hedhi, maumivu wakati wa kukojoa na wakati wa kujisaidia haja kubwa. 

Mengine yanatajwa kitaalamau, ni kuwa na ukavu kwenye sehemu za siri, kupata maumivu ya mgongo, kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa au baada ya kujamiiana. 

Pia, inatajwa kuna wakati mwanamke mwenye dalili hizo huwa anahisi hali ya kichefuchefu na kutapika kama mjamzito, homa kali, uchovu, kizunguzungu na kukosa hamu ya kula. 

UTAMBUZI NA TIBA  

Jinsi ya kutambua mgonjwa wa PID, ishara kuu ni utambuzi wa ugonjwa huo hutokana na dalili za mgonjwa, daktari anafanya uchunguzi wa sehemu za siri za mgonjwa.  

Namna ya uchunguzi na anachotambua tabibu, ndicho kinachoamua kuchukuliwa sampuli za maji au usaha kutoka sehemu za siri, ili kutambua aina ya vimelea anayesababisha maambukizi na ugonjwa. 

Madhara ya ugonjwa wa PID kwa mwanamke, yanaweza kusababisha maambukizi katika viungo vya uzazi na kusababisha ugumba au kutokuwa na uwezo wa kupata ujauzito. 

Inaelezwa, namna mgonjwa anavyozidi kukaa na hali hiyo au kupata maambukizi kwenye njia ya uzazi, ndiyo hatari ya ugumba inazidi kuongezeka na uwezekano wa kutopata mtoto baada ya hapo. 

Hali ya kutunga mimba nje ya kizazi nayo inachangiwa na ugojwa huo. Mimba huweza kutunga nje ya kizazi, endapo maambukizi hayo yamesababisha makovu ndani ya mirija ya uzazi. 

Makovu hayo husababisha yai lililopevushwa kushindwa kusafiri ndani ya mirija ya uzazi kuelekea kwenye mji wa uzazi. 

Mimba nje ya uzazi, husababisha utokaji wa damu usio wa kawaida ambao hatari yake unaweza kukatisha uhai wa mwanamke.

Ugonjwa huo kitaalamu unaelezwa unaweza kusababisha shida nyinginezo; maradhi ya ‘Kansa ya Shingo ya Kizazi’ au uvimbe kwenye mayai ya mwanamke. 

Mvurugiko wa homoni nao huweza kusababisha mwanamke kupata hedhi ya muda mrefu au kukosa kuona hedhi kabisa.

Hapo napo inajitokeza suala la maumivu ya tumbo chini ya kitovu. Mwanamke mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, huwa anasumbuliwa kila mara na maumivu chini ya tumbo.

HATUA ZA KINGA

Hata hivyo, inatajwa kuna njia za awali za kujikinga na ugonjwa huo, pale mwanamke anahimizwa kuwa na mpenzi au mwenza mmoja, na akijua historia yake ya mahusiano yaliyopita, kutumia kinga wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Mwanamke anashauriwa kumshauri mwenza wake kupima afya yake dhidi ya magonjwa ya zinaa, pia virusi vya Ukimwi, kabla ya kuanzisha uhusiano naye. 

Hata hivyo, daktari wa kinamama wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, Benjamini Kimaro, anashauri kitabibu mwanamke mwenye maradhi ya PID, hatua bora ni vema hatua yake ya awali ni kuwahi kwenye kituo cha afya ili apate tiba na kuepuka madhara kama ya ugumba.

Dk. Kimaro anasema, jamii nayo kwa ujumla inapaswa kutambue kuopata elimu ya chanzo kikuu chja maradhi PID na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa, katika jitihada za kuepuka ugonjwa huo.

Hapo ni namna inayoacha ujumbe wenye kipaumbele kwa wanawake wa Kitanzania, washirikiane kupeana elimu  na maelekezo kwa watoto wa kike, hali itakayosaidia kuepusha ugonjwa huo.

Mtazamo na ujumbe mahsusi ni kwamba; “unapomuelimisha mtoto wa kike, unakuwa umekita kwenye mizizi au kiini cha ugonjwa huo”, kwani watakuwa chachu au msaada kwa wengine.

*Makala hii ni kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya afya.