BABA mzazi wa nahodha wa timu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyefariki juzi, Ally Samatta Pazi, anatarajiwa kuzikwa leo Jumatatu kijijini kwao Kibiti Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Mohammed Samatta, mwili wa Mzee Samatta utaondoka nyumbani kwake Mbagala jijini Dar es Salaam leo asubuhi kuelekea Rufiji kwa maziko.
“Mwili wa marehemu baba yetu, Mzee Ali Pazi utasafirishwa kesho (leo Jumatatu) kwenda kuzikwa nyumbani kwao Kibiti, Rufiji,” alisema Mohammed.
Kwa mujibu wa Mohamed baba yake alifariki baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Samatta ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi Tanzania, enzi zake alikuwa mchezaji mzuri wa nafasi ya ushambuliaji ambaye alichezea hadi timu ya taifa ya Tanzania, Taia Sars kuanzia mwaka 1964 hadi 1965.
Alizaliwa Oktoba 28 mwaka 1943 na umaarufu wake katika soka ulianza alipokuwa anasoma sekondari ya Mzumbe mkoani Morogoro kwenye michezo ya Shule kati ya mwaka 1961 na 1962 na mwaka 1963 akaajiriwa Jeshi la Polisi Tanzania na kuanza kuchezea timu ya jeshi hilo Jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1965 alisajiliwa na Cosmopolitan ya Dar es Salaam aliyoichezea hadi mwaka 1966 akarejea Polisi na mwaka 1968 akasajiliwa na Sunderland, sasa Simba SC ambako alicheza kwa miezi kadhaa kabla ya kurejea Polisi kufuatia kuhamishiwa kikazi mkoani Mara.
Alicheza Polisi Mara kwa mwaka mmoja hadi 1969 alipohamia kikazi Bukoba na kiuchezea Polisi Kagera hadi mwaka 1973 alipohamia Polisi Morogoro, hadi 1975 akarejea Polisi Mara hadi 1980 akahamia Polisi Shinyanga hadi alikodumu kwa miezi michache akahamishiwa Polisi Tanga ambako alistaafu mwaka 1992.
Mzee Samatta alikuwa mtu mashuhuri katika jamii yake, akiheshimika kwa malezi bora aliyowapatia watoto wake, hasa Mbwana ambaye amekuwa nembo ya soka la Tanzania kimataifa.
Marehemu aliwahi kuelezea namna alivyomlea mwanawe katika maadili, nidhamu na upendo na kulitumikia taifa lake, mambo ambayo bado yanaonekana katika mwenendo wa nyota huyo wa soka.
Ni pengo kubwa kwa familia, lakini pia kwa taifa ambalo limemshuhudia baba huyo akiwa bega kwa bega katika mafanikio ya mwanaye uwanjani.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED