Fadlu ataka tisa wa kigeni Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:21 PM Jul 07 2025
news
Picha Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids

MOJA ya kazi iliyofanywa na kikao cha Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Bodi ya Ushauri chini ya Mwenyekiti, Mohamed Dewji, hivi karibuni ni kupitia ripoti ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kuwapa watu majukumu ya kusaka wachezaji watakaojaza maeneo yaliyoainishwa kuwa yana mapungufu, huku viongozi wa zamani waliokuwa wakileta wachezaji wa viwango vya hali ya juu nao wakihusishwa.

Taarifa zinasema kuwa, pamoja na mambo mengine, Fadlu ameainisha maeneo kadhaa, huku akitaka wachezaji wasiopungua sita wa kigeni, wengine wa hapa nchini, kazi hiyo ikiwahusisha baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo ambao waliweza kufanya usajili mkubwa kama wa kina, Juma Kaseja, Mussa Hassan Mgosi, Nico Nyagawa, Emmanuel Gabriel, Patrick Mafisango, Emmanuel Okwi, Macky Sirengo, Shiza Kichuya na wengine wengi, licha ya kuwa hawakuwa na fedha nyingi zanusajili.

"Kocha ametaka Jean Charles Ahoua aongezewe nguvu, yaani kuwe na mchezaji mwingine kwenye namba 10 pale ambaye anaweza kufunga na kutoa asisti, anahitaji beki wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kukaba kwa nguvu na akili pia, kiungo mkabaji mwenye ubora kushinda Yusuph Kagoma.
“Winga mwenye uwezo mkubwa kuliko Joshua Mutale, na mashambuliaji mmoja au wawili wenye uwezo mkubwa wa kupachika mipira ndani ya wavu, kuliko Leonel Ateba na Steven Mukwala," kilisema chanzo.

Hata hivyo, Mulate, Ateba na Mukwala, wote wanaweza kuwa si sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao.

Mukwala ambaye amemaliza mkataba wa Simba, huenda akatimkia, Kaizer Chiefs, huku Ateba na Mutale wakioneshewa mlango wa kutokea kutokana na kutokidhi matakwa ya klabu na kocha Fadlu pia.

Taarifa zinasema kuwa huenda Simba ikapata wachezaji wazuri zaidi msimu ujao, kwani katika shughuli hiyo wamehusishwa baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo ambao walikuwa wakisajili wachezaji wasio na majina makubwa, lakini waliokuwa na uwezo mkubwa, wengi wakiwa kwenye Bodi ya Ushauri.

Wajumbe wengi wa Simba wenye uwezo wa kufanya usajili, wapo kwenye Bodi ya Ushauri inayoundwa na watu wengi waliokuwa viongozi wa klabu hiyo zamani.

"Unajua watu kama kina Geofrey Nyange 'Kaburu', Hassan Dalali, Ismail Aden Rage, Evance Aveva, hawakuwa na pesa nyingi sana, lakini walikuwa na uwezo mkubwa wa kusajili, walikuwa na jicho la kuona wachezaji bora ndani na nje ya nchi.

“Hawakushirikishwa kwenye usajili wa msimu uliopita, lakini huu unaokwenda kufanya na wao wapo, walikuwemo kwenye kikao, wamemshauri mwenyekiti wetu nini cha kufanya ili kupata kikosi chenye ubora na tishio," alisema mtoa taarifa.

Baadhi ya wachezaji ambao Simba huenda ikawanasa msimu ujao na imekuwa kwenye mazungumzo nao ni, Feisal Salum wa Azam FC,  Lassine Kouma, kiungo mshambuliaji raia wa Mali kutoka Stade Malien, Abdallah Kulandana, kiungo mkabaji kutoka Fountain Gate, Owen Tembo.

Pia kiungo mkabaji kutoka Power Dynamos ya Zambia, Abdou Seyd, raia wa Senegal, kiungo mkabaji anayekipiga kwenye klabu ya Tunisia, Ousine Badamasi, kiungo mshambuliaji raia wa Nigeria na Balla Conte, raia wa Guinea, anayeichezea klabu ya Sfaxien ya Tunisia.

Mbali na hayo, Simba pia iko kwenye mazungumzo na wachezaji wawili wa JKT Tanzania, Yacoub Suleiman, beki wa kati, Wilson Nangu na Karim Mfaume Bakari, lakini vile vile ikiwawinda, Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo wote wa Azam FC.