KLABU ya Yanga imesema tayari imempata Kocha Mkuu atakayeifundisha timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano, lakini haitomtangaza hadi hapo itakapomaliza zoezi la usajili ambalo yeye ndio analisimamia.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema kazi iliyokuwepo sasa ni kuandika barua za kuachana na wachezaji ambao hawatokuwa nao kwa msimu ujao, wakitarajia kuanza kuzitoa wiki ijayo.
Kamwe, alisema baada ya zoezi hilo, wataanza kuzungumza na wachezaji wanaowahitaji ambao wamemaliza mikataba wao ili kuwaongezea.
Vyanzo vinasema Yanga imebaki mkononi na majina mawili ya makocha baada ya mchujo mkali, ambao ni Julien Chevalier raia wa Ufaransa, anayeifundisha Asec Mimosas ya Ivory Coast na Rhulani Mokwena, raia wa Afrika Kusini, aliyekuwa kocha wa Wydad Casablanca ya Morocco, hivyo mmoja wao ndiye atakayetangazwa kuwa kocha mkuu.
"Kocha Mkuu ameshapatikana, atakuja na baadhi ya watu kwenye benchi letu, tumesimama kidogo kumtambulisha kwa sababu tupo katika kipindi muhimu cha usajili.
“Tunataka kumshirikisha kwenye usajili ili isije baadaye kama mambo yatakuwa mabaya aseme kama hakushirikishwa, sisi huwa tunawashirikisha makocha wetu ndiyo maana mara nyingi tunafanikiwa.
“Tutashirikiana naye, kazi hiyo ikishakamilika tutakuja kumtambulisha na wanachama na mashabiki watamfahamu," alisema Kamwe.
Alisema awali tayari walikuwa na majina ya wachezaji waliopendekezwa kusajiliwa ambao yametokana na ripoti ya benchi la ufundi lililopita, lakini wameona si busara kuendelea kufanya hivyo kabla kocha mpya hajaweka nguvu zake.
"Ukweli ni kwamba hatujaanza usajili, yapo majina ya wachezaji tunayo kutoka ripoti iliyopita, lakini tukasema si busara kuendelea na usajili kabla kocha mpya hajaweka mawazo, ushauri na nguvu zake, akifanya hivyo uongozi sasa ndiyo utaanza kuufanyia kazi,"alisema.
Kamwe aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kutokuwa na wasiwasi kwani mara zote huwa makini sana linapokuja suala la kuboresha kikosi.
"Wanachama na mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi, mara zote sisi huwa makini sana linapokuja suala ya kuboresha timu yetu, tutaanza na kubakisha wachezaji bora tuliokuwa nao, halafu tunaongeza wengine ili kuweza kufikia malengo ya msimu ujao.
“Nikuibieni siri ni kwamba, kocha wetu mpya anaifahamu vizuri Yanga, kwa hiyo haitomuwia vigumu, ukiona mchezaji amebaki ujue kocha anataka kutumia, ukiona kaondoka ujue hamhitaji.
“Kufika wiki ijayo tutakuwa tumewapa barua wale ambao hatuwahitaji, wale tunaotaka kuwaongeza mikataba tutaanza kuzungumza nao, huku usajili ukiendelea chini ya kocha mpya anayechukua mikoba ya Miloud Hamdi.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED