Jukwaa lawakutanisha wakulima 500 kujadili kukuza sekta ya kilimo

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:27 PM Apr 12 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza na wakulima wakati wa jukwaa la ushirika lililofanyika mjini kahama leo.
PICHA: SHABANI NJIA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza na wakulima wakati wa jukwaa la ushirika lililofanyika mjini kahama leo.

JUKWAA la Ushirika la mkoa wa Shinyanga, limewakutanisha wakulima zaidi ya 500 wa mazao ya chakula na biashara kutoka Vyama vya msingi (AMCOS) 299, kujadili namna ya kukuza sekta ya kilimo ili izidi kuwanufaisha na kuondokana na umasikini.

Aidha, wakulima hao ni kutoka katika vyama vya msingi ambavyo ni wanachama wa Vyama Vikuu viwili vya Ushirika mkoa wa Shinyanga-SHIRECU pamoja na KACU Wilaya ya Kahama, na kusisitizwa kuzalisha mazao yao kwa tija ambayo yatakuwa na ushindani katika masoko ya kimataifa.

 Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ambae ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika-KACU Emmanuel Nyambi amewakutanisha wakulima hawa leo huku akisisitiza kila mwaka wamekuwa wakikutana na kujadili changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi na zile zilizopo nje ya uwezo wake wanazizalisha wizarani.

 Amesema,wamekutana zaidi ya wakulima 500 kutoka vyama vya msingi 299 kuweka mikakati Madhubuti ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na itawafanya kukua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

 “Jukwaa hili limetukutanisha kueleza changamoto zinazotukabili na zinazoukabili ushirhirika ili kuzijadili kwa pamoja nakupata suluhisho, Ushirika ndio chombo pekee kinachounganisha wakulina wote nchini na wakunufaika na kilimo” Amesema Nyambi.

 Mwakilishi kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCu) Dk. Gratian Rwekaza ametoa mada juu ya fursa za ushirika kwenye soko huria katika kukuza uchumi wanachama na jamii na kuwasisitiza kulima kwa tija na kuanzisha vyanzo mbadala na kuacha kuendelea kutegemea ushuru pekee.

Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim, amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni ushirika hujenga ulimwengu ulio bora na vyama vimekuwa vikiwasaidia wanachama wake kupata pembejeo na viuatilifu kwa wakati.

 Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amesema viongozi wanatakiwa kufuata kanuni na sheria za ushirika kwani wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakishindwa kusimamia ushirika, kutoa maamuzi na kusababisha kuibuka kwa migogoro.

 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha ameushauri uongozi wa chama cha ushirika Kacu kuungana kwa pamoja kukifufua chama cha Ushirika Shirecu ili kiweze kulipa madeni kinayodaiwa na kuamini na kuanza kukopeshaka na taasisi za kifedha ilivyokuwa hapo awali.

Pia amewataka wakulima wa zao la pamba kuacha mara moja tabia ya kuchanganya pamba mbegu na mchanga wakati wa masoko ili kuongeza uzito kwani inaua soko la kimataifa na kushuka bei na kuitangaza nchi kuwa na sifa mbaya ya kuwa na pamba chafu kila msimu.