Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosiamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha anatatua kero mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini mkoani Simiyu, ambao wameonyesha kuridhishwa na hatua hiyo.
Akizungumzia katika mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini mkoani humo, Kihongosi amesema changamoto kubwa iliyokua inaikabili kada hiyo ni ukosefu wa mitaji na kufanya utafiti wa maeneo yaliyoko madini.
"Tayari serikali kupitia Wizara ya Madini imeunda Tume Maalum kati ya sekta binafsi na ya umma ili kufuatulia changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo ikiwemo kuangalia namna wanavyoweza kuwezeshwa mitaji na mbinu za utafiti," amesema Kihongosi.
Kuhusiana na umeme ambao ni hitaji la msingi katika maeneo ya Migodi, kiongozi huyo amesema, tayari serikali imetoa Sh. Bilioni 90 ili kujenga kituo cha kuongeza nguvu ya umeme kwa lengo la kumaliza changamoto ya umeme kukatika mkoani Simiyu huku wakiwapunguzia wachimbaji gharama ya kutumia mafuta ya diesel.
Naibu Waziri wa Madini Dk. Steven Kiruswa amesema serikali itaendelea kufuatilia na kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji nchini lengo likiwa ni kutoa kipaumbele cha kipekee kwa wachimbaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED