“Serikali yatenga asilimia 30 za zabuni kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu”

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:17 PM Jun 17 2025
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete, amesema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika zabuni za ununuzi wa umma kwa kutenga rasmi asilimia 30 ya zabuni hizo kwa ajili yao.

Ridhiwan ameyasema hayo jana Juni 16, 2025, alipohutubia Kongamano la Ununuzi wa Umma lililoandaliwa na PPRA jijini Arusha, likiwa na lengo la kujadili nafasi ya makundi maalum kwenye ukuaji wa uchumi jumuishi katika zama za mabadiliko ya teknolojia.

Katika taarifa yake alisema: 
“Nimewakumbusha umuhimu wa kuendelea kutambua kuwa mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita yanalenga pamoja na mengineyo kuwasaidia na kukuza ustawi wa watu wenye mahitaji maalum,” 

Alisisitiza kuwa mbali na kutenga asilimia 30 za zabuni, bado kuna haja ya kuongeza elimu kwa jamii kuhusu upatikanaji wa fedha hizo, akiwataka viongozi wa serikali za mitaa, madiwani na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia wananchi.

“Umuhimu na msisitizo kama huu umesaidia sana vijana, wanawake na wenye ulemavu kukimbilia zile asilimia 10 zinazotengwa na halmashauri kutoka kwenye mapato ya ndani,” aliongeza.

Akiwaaga washiriki wa kongamano hilo, Ridhiwan aliipongeza PPRA kwa kuandaa jukwaa hilo muhimu kwa maendeleo ya Watanzania wote.