Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) limeanza kuvijengea uwezo vyombo vya habari nchini ili kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na kupambana na tatizo la udumavu kwa rika zote, kwa lengo la kupunguza mzigo kwa serikali.
Mafunzo hayo yameanza kutolewa hivi karibuni kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa PANITA, Tumaini Mikindo, alisema lengo ni kuviongezea uelewa vyombo hivyo kuhusu umuhimu wa kukuza lishe bora nchini (Nutrition for Growth), mipango ya sasa ya serikali na nafasi ya wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa wajawazito, watoto na watu wa rika mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mikindo, mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kwa wanahabari kuhusu lishe na nafasi yao katika shughuli za kila siku za kuboresha hali ya lishe nchini.
Mratibu wa Programu wa PANITA, Jane Msagati, akizungumza katika mafunzo hayo, alisema siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto ni muhimu katika kuhakikisha anakuwa na afya bora. Alibainisha kuwa kipindi hicho ni muhimu kwa kuboresha lishe ya mtoto hadi anapofikia utu uzima.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu hali ya lishe nchini, Ofisa Utafiti Mchumi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Geoffrey Chiduo, alisema sekta ya afya na sekta nyingine zinapaswa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya udumavu ambao ni tishio kwa jamii na nguvu kazi ya taifa.
Chiduo alionya kuwa ikiwa hali ya lishe duni ya watoto itaendelea, kuna hatari ya Tanzania kuwa na watu milioni 840 wenye aina fulani ya utapiamlo kati ya watu bilioni 1.5 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na TFNC, limeweka malengo ya kuhakikisha kuwa tatizo la utapiamlo linalotokana na lishe duni linatokomezwa nchini ifikapo mwaka 2030.
Alibainisha kuwa miongoni mwa mikakati ya kitaifa na kikanda inayotekelezwa ni pamoja na kupunguza aina zote za utapiamlo, kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza baada ya mtoto kuzaliwa, kuhakikisha uhakika wa chakula, kuongeza utashi wa kisiasa na uwajibikaji, pamoja na kuwekeza zaidi kwenye sekta ya lishe.
Chiduo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 66 zilizojiunga na mpango wa kimataifa wa kukabiliana na utapiamlo. Mnamo mwaka 2017, viongozi wa dunia walikutana jijini Milan, Italia, na kuahidi kutoa dola bilioni 3.4 kwa ajili ya kuboresha lishe. Aidha, mwaka 2021 wadau walikutana tena katika kongamano la Tokyo, Japan, kuendeleza jitihada hizo.
Kwa mujibu wa Chiduo, katika kongamano la mwaka huu 2025 lililofanyika Paris, Ufaransa, Umoja wa Ulaya (EU) uliahidi Euro bilioni 6.5, Benki ya Dunia (WB) dola bilioni 5, na Serikali ya Ireland kutoa ahadi mpya katika mapambano dhidi ya utapiamlo duniani.
Kwa upande wao, waandishi wa habari walishukuru PANITA kwa mafunzo hayo na kuomba yawe yanafanyika mara kwa mara ili kuwasaidia kuwa sehemu ya kutokomeza utapiamlo nchini.
Takwimu zilizotolewa na PANITA zinaonyesha kuwa inakadiriwa asilimia 59 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa damu, asilimia 30 wakiwa na udumavu wa kawaida, asilimia 4 wakikabiliwa na uzito uliozidi, na asilimia 3.3 wakiwa na ukondefu uliopitiliza kutokana na lishe duni.
Aidha, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya udumavu kwa watoto duniani, ikifikia asilimia 30. Mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha udumavu kwa watoto ni Rukwa, Njombe na Iringa kwa zaidi ya asilimia 50, huku Katavi, Geita, Ruvuma, Simiyu na Tabora ikiwa na wastani wa kati ya asilimia 30 hadi 40.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED