Wanafunzi Mwanalugali wapata samani za Bwalo za milioni 10

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 02:29 PM Jun 17 2025
Wanafunzi Mwanalugali  wapata samani za Bwalo  za milioni 10
Picha:Mpigapicha Wetu
Wanafunzi Mwanalugali wapata samani za Bwalo za milioni 10

Hatimaye wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kata ya Tumbi, Halmashauri ya Mji Kibaha, wanakwenda kuondokana na kero ya kula chakula wakiwa wamesimama baada ya shule hiyo kupokea msaada wa Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa samani za bwalo.

Taasisi ya Fedha inayojihusisha na mikopo ya nyumba (TMRC) imekabidhi fedha hizo kwa uongozi wa shule kwa ajili ya ununuzi wa samani za bwalo la chakula ili kuondoa adha hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya fedha hizo iliyofanyika shuleni hapo Juni 16, Mkuu wa Shule hiyo, Uyeka Kessy, amesema kupatikana kwa msaada huo kumetokana na jitihada za mdau wa maendeleo, Dk. Charles Mwamwaja, ambaye walimueleza mahitaji hayo.

Amemshukuru mdau huyo kwa kutafuta wafadhili waliowezesha upatikanaji wa fedha hizo za kununua samani za bwalo la chakula, huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kutatua changamoto nyingine za shule hiyo ikiwemo ujenzi wa uzio.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Alex Lubawa, amesema kwa sasa shule hiyo ina uhitaji mkubwa wa uzio, ambao ukijengwa utasaidia kudhibiti utoro kwa wanafunzi.

Naye Dk. Charles Mwamwaja, ambaye pia ni Kamishna wa Wizara ya Fedha na mkazi wa Mwanalugali, Wilaya ya Kibaha, amesema amekuwa akiguswa na maendeleo ya jamii, hususan yanayogusa elimu.

Amesema wanafunzi wanapaswa kusoma katika mazingira rafiki, yakiwemo maeneo mazuri ya kula chakula, viwanja vya michezo, na vyumba vya madarasa.

Dk. Mwamwaja amesisitiza kuwa wadau wa maendeleo ni sehemu muhimu ya kusaidia serikali kutatua changamoto za kijamii, na wataendelea kushirikiana na serikali kuondoa vikwazo vya maendeleo.

Ameongeza kuwa kwa lengo la kuinua ufaulu wa wanafunzi hao na kuwawezesha kufikia malengo yao, ipo programu maalum iitwayo Safari Yangu Kielimu (SYK) ambayo itasaidia kuwajengea uwezo wanafunzi kujiamini kwa kuwakutanisha na watu waliowahi kufanikiwa kupitia changamoto za shule.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya, amesema zipo shule nyingi zenye mahitaji kama hayo, na kwamba ujio wao shuleni hapo umetokana na maombi kutoka kwa mdau huyo wa maendeleo.

Mgaya amesema taasisi hiyo imeguswa na changamoto ya shule hiyo na imeamua kuchangia Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kusaidia kupunguza changamoto hizo, ikiwemo upatikanaji wa meza na viti kwa ajili ya bwalo la chakula.