SERIKALI imetoa Sh. bilioni 78.88 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kujifunza na kufundishia katika kampasi sita kati nane za Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Pili cha Baraza la Kuu la Wafanyakazi wa taasisi hiyo, kilichofanyika mkoani Morogoro.
Amesema taasisi hiyo, imekusudia kuliteka soko katika nchi za Afrika, lenye ushindani kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora ya uhasibu na kuwa kivutio.
“Mpango wa ukarabati wa kampasi hizo sita umelenga kuhakikisha TIA inakuwa miongoni mwa taasisi kubwa za elimu na zenye mazingira wezeshi, yatakayovutia soko la ndani na nje ya nchi katika kutoa huduma bora za kisasa ambazo zitaleta ushindani na taasisi zingine za nje.”
Prof. Pallangyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo TIA, alizitaja kampasi hizo zinazoboreshewa miundombinu ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia ni zilizopo mikoa ya Singida, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Zanzibar na kwamba zitakuwa za kisasa, kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
“Pamoja na kampasi ambazo zinafanyiwa ukarabati wa miundombinu hiyo ambazo ni sita lakini tunazo nyingine mbili ambazo ni Dar es Salaam na Tanga ambazo kwa ujumla kwa sasa tuna wanachuo 31,106 tunaiskuru sana serikali kwa sababu lengo la taasisi ni kusogeza huduma na wananchi” amesema Pallango.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la TIA, amesema mpango huo wa Serikali pia umekwenda sambamba na kuendeleza na kuwagharamia masomo wahadhiri wa shahada ya uzamivu 32 na ngazi ya shahada ya uzamili ambao tayari jumla yake 41 wamehitimu masomo ya shahada ya uzamivu.
Akifunguza Baraza hilo la TIA, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk Mussa Alli Mussa, amesema kwa sasa fani ya uhasibu ina ushindani mkubwa wa soko la ndani na nje ya nchi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia hivyo ni muhimu wakaenda na kasi hiyo, ili kuitangaza Tanzania kimataifa.
Dk. Mussa, amesema aahasibu nao wanayo nafasi ya kuongeza ujuzi ulio nje ya taaluma yao kutokana na ushindani uliopo, ili waweze kupata maarifa zaidi na kuweza kuingia kwenye ushindani wa soko kwenye nchi zinazoendelea.
“Tunapozungumzia kesi kuhusu Data analysis,na elimu nyingine zinazohusianana mambo hayo,kama si wahasibu wasipokuwa na uwezo wa uchambuzi wa data watakuwa wanaburuzwa na kushindwa kuhimili soko lenye ushindani hivyo lazima wajiongeze tu hakuna namna,” amesema Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Morogoro.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la TIA, Magreth Muhamaso, amewataka wafanyakazi wote kusimamia sheria na miongozo mbalimbali ya utekelezaji inayotolewa, ili kuifanya taasisi hiyo iweze kupata mafanikio kitaifa na kimataifa na kuleta ushindani kwa wahitimu wake kugombewa kwenye soko la ajira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED