Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamepongezwa kwa kuandaa na kuendesha kwa mafanikio makubwa mkutano mkuu wa mwaka.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo imewawezesha kujadili kwa kina taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na kuweka mapendekezo yenye lengo la kuongeza tija ndani ya TCAA.
Akifungua mkutano huo wa siku mbili unaofanyika jijini Dodoma leo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Amani Msuya amewapongeza viongozi wa TUGHE TCAA kwa uendeshaji mzuri na shirikishi wa shughuli za chama hicho, akieleza kuwa tawi hilo limekuwa mfano bora wa kuigwa na matawi mengine.
"Nawasihi viongozi waendelee kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE kwa sababu huo ndio uhai wa chama. Bila wanachama hai, hakuna chama hai. TCAA mmeonyesha njia nzuri, endeleeni kushikamana na kushirikiana," amesema Msuya.
Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Sara Rwezaura amewataka wanachama wa TUGHE TCAA kuwa wavumilivu wakati wa kuwasilisha hoja zao, na kusisitiza kwamba hoja zao ni muhimu na zisikaliwe kimya bali ziwasilishwe kwa mujibu wa taratibu.
Pia Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA, Jackline Ngoda amewashukuru viongozi wenzake kwa kuendelea kudumisha mshikamano ndani ya uongozi na kuahidi kuongeza nguvu katika kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE.
Naye, Katibu wa TUGHE TCAA, Shukuru Mhina amesisitiza umuhimu wa mafunzo kwa viongozi wapya wa TUGHE akieleza kuwa ni kupitia mafunzo ndipo viongozi bora hujengwa.
Mkutano huo wa mwaka wa TUGHE TCAA umeendelea kuonesha mfano wa uwajibikaji, mshikamano na ushirikishwaji, hali inayoendelea kuimarisha misingi ya utendaji bora ndani ya taasisi hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED