BAADHI ya wakazi wa Kata ya Lembeni wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro wamesema kushuka wa ari ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika maeneo yao kunatokana na wakulima kushindwa kumudu gharama za kununua dawa na mbolea kwa ajili ya kustawisha mazao.
Badala yake, wanaona kilimo ikolojia (kilimo hai) kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa wakulima kama serikali na wadau wa wa sekta ya kilimo watawapa elimu wakulima kubadili aina ya uzalishaji wa mazao ya chakula.
Mkazi wa Lembeni, Janeth Mshana, akizungumza jana na NIPASHE katika mahojiano maalum kuhusiana na mpango wao wa kujikita zaidi kwenye kilimo ikolojia, alisema nguvu kubwa inayotumika kuhudumia mashamba kuua wadudu na magonjwa kwenye mazao yao kwa kutumia kemikali ni mzigo kwa wakulima wengi.
“Tunatumia kilimo cha kisasa, ambacho kinatuletea mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababishwa na kutumia dawa za kemikali katika kilimo kwenye mazao; kitu ambacho kinachangia ardhi kupoteza rutuba yake,” alisema.
Paulo Msangi, alisema iko haja kwa serikali na wadau wa kilimo hai nchini kuweka katika mipango yao mbegu stahimilivu kwa uhakika wa chakula lishe na kuongeza kipato.
Tayari Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania, wameanzisha kampeni ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu kilimo ikolojia katika Kata hiyo na za Maore na Vumari Wilaya ya Same.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisema eneo la kilimo ikolojia linahitaji msukumo wa wadau ili kuhamasisha wanawake kushiriki katika kilimo hicho na kukipa uzito katika jamii.
Alisema kilimo hicho kina tija kubwa licha ya kuwa ni cha asilia kwa sababu hakitumii dawa za kemikali.
Alisema serikali imetambua umuhimu wa kilimo hicho na kwa sasa kuna juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha wakulima wanapata tija.
Alitoa mfano kuwa serikali imeanzisha idara ya kilimo ikolojia katika Wizara ya Kilimo na dawati mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha kilimo hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED