Wizara ya Viwanda yataka CBE izalishe wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:42 AM Jun 21 2025
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.

Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa taasisi za elimu zinatoa mafunzo yanayozalisha wahitimu wenye uwezo wa kuzalisha ajira kwa wengine badala ya kusubiri kuajiriwa.

Kauli hiyo aliitoa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Exaud Kigahe mwishoni mwa wiki wakati wa kongamano la kuimarisha fursa za ajira na maendeleo endelevu ya Tanzania kaulimbiu ikiwa ni ‘ubunifu na ujasiriamali kwa ajira endelevu’

Alisema  CBE imejidhihirisha kwa kuanzisha programu kama Atamizi za Biashara na Uanagenzi, ambazo zimekuwa chachu ya kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo na kuwaunganisha moja kwa moja na waajiri.

Alisema kupitia programu ya atamizi za Biashara, vijana wanaweza kukuza mawazo

yao ya kibunifu na kuunda biashara zinazoweza kutoa ajira kwa wenzao.

Aidha, alisema mpango wa uanagenzi umefanikiwa kuwaweka wanafunzi wa CBE katika mazingira halisi ya kazi, wakijifunza kwa vitendo kabla ya kuhitimu.

“Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi, Chuo kimezindua Dira ya Maendeleo ya Miaka 50 – CBE Vision 2075, inayolenga kukifanya kuwa taasisi ya mfano katika kuzalisha wahitimu bora, wabunifu, na wenye uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa,”

“ Dira hii inaweka bayana mwelekeo wa chuo katika kuimarisha ajira kwa wahitimu, kukuza ubunifu, kuendeleza elimu kwa vitendo, na kuandaa vijana kwa ajira za kidijitali za sasa na baadaye kwa hiyo napenda kusisitiza kwa kuwa utekelezaji wa dira hii ni jukumu la Chuo kikisimamiwa na usimamizi wa Bodi ya Uongozi wa chuo,” alsiema

Aidha, Waziri alisema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iko tayari kuendelea kushirikiana na CBE kuhakikisha dira hii kutosalia kwenye karatasi, bali inatekelezwa kwa vitendo na mipango thabiti, na kutoa matokeo yanayoonekana kwa vijana na Taifa kwa ujumla.

Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kutengeneza fursa nyingi zaidi za ajira kwa kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za elimu kama CBE.


“Tunahakikisha mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuongeza uzalishaji wa viwanda, uongezekaji wa biashara, na hatimaye kupanua wigo wa ajira kwa vijana wa Kitanzania, kupitia Kongamano hili, nawahimiza waajiri na wadau wa sekta ya biashara kushirikiana na taasisi za elimu ili kutengeneza mfumo unaowaandaa wahitimu kwa mahitaji halisi ya soko,” alisema.

Alisema viwanda vinapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa ajira kwa Watanzania na kusaidia mafunzo ya kiufundi ili kuongeza ujuzi wa wafanyakazi. na kwamba Serikali ya awamu ya sita itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha inajenga mazingira bora ya ajira na mafunzo kwa vijana .

“Ni lazima tujenge daraja imara kati ya elimu na ajira, ili kuhakikisha kuwa Taifa letu linaendelea kuwa na nguvu kazi bora, yenye maarifa, na inayoweza kushindana kimataifa,” alisema.

“Tunapowekeza katika elimu yenye kuzingatia ujuzi na ubunifu, tunajenga msingi wa uchumi imara unaotegemea nguvu kazi yenye maarifa na utayari wa kujiajiri. Kwa msingi huo, Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na CBE katika kuhakikisha kuwa Kongamano hili linakuwa jukwaa la kudumu la kuendeleza ajira na kujenga uchumi wa Taifa,” alisema.