Trump: Ulaya inaporomoka na viongozi wake ni dhaifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:10 PM Dec 10 2025
news
Picha Mtandao
Trump: Ulaya inaporomoka na viongozi wake ni dhaifu

RAIS wa Marekani Donald Trump amewakosoa viongozi wa Ulaya kwa kuwaita dhaifu na kusema Marekani inaweza kupunguza msaada kwa Ukraine.

Katika mahojiano ya kina na mtandao wa habari Politico, Trump amesema nchi za Ulaya dhaifu zimeshindwa kudhibiti uhamiaji au kuchukua hatua madhubuti kukomesha vita vya Ukraine na Urusi, akiwashutumu kwa kuiacha Kyiv ipigane hadi ianguke.

Aidha, anaelezwa kuwa viongozi wa Ulaya wamefanya majaribio ya kuonyesha jukumu katika juhudi zinazoongozwa na Marekani za kukomesha vita hivyo, ambavyo wanahofia vitaathiri maslahi ya muda mrefu ya bara hilo kwa ajili ya suluhisho la haraka.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Uingereza Yvette Cooper amesema alichokiona barani Ulaya ni uimara, akitoa mfano wa uwekezaji katika ulinzi pamoja na ufadhili kwa Kyiv.

Aliongeza kuwa marais wawili walikuwa wakishughulikia mchakato wa amani akimrejelea Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky huku Rais wa Urusi Putin hadi sasa akiendelea kuzidisha mgogoro huo kwa kutekeleza mashambulizi zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora.

Trump ameelekeza shinikizo kwa Zelensky kuunga mkono makubaliano ya amani, akimhimiza kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa kukabidhi eneo kwa Moscow.

Urusi ilizindua uvamizi wake kamili nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

Zelensky, akiandika kwenye mtandao wa X baadaye Jumanne, amesema Ukraine na Ulaya zilikuwa zikifanyia kazi kikamilifu vipengele vyote vya hatua zinazowezekana ili kukomesha vita, na kwamba vipengele vya Ukraine na Ulaya vya mpango huo sasa vilikuwa vimeendelezwa zaidi.