14 'wamvaa' Prof. Muhongo ubunge Musoma Vijijini, yumo mwana mama

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:27 PM Jul 01 2025
Profesa Sospeter Muhongo.
Picha: Mtandao
Profesa Sospeter Muhongo.

Makada 14 wa CCM wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya kupitishwa kuwania ubunge wa Musoma Vijijini mkoani Mara, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, jimbo hilo limekuwa likiongozwa na Profesa ambaye naye amejitosa kwenye king'anyiro ili kutetea nafasi yake hiyo.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya ya Musoma, Elisante Kimaro, hadi kufikia jana makada ambao tayari walikuwa wamechukua  fomu walikuwa ni 15, akiwamo Profesa Sospeter Muhongo.

Hata hivyo, alikataa kutaja majina yao akidai kuwa ni siri ya chama. "Majina ya wagombea hayawezi kuwekwa wazi," amesema Kimaro na kukata simu. Lakini katika mitandao ya jimbo hilo, kuna picha mbalimbali za watia nia wakipokea fomu kutoka kwa katibu huyo.

Baadhi ya picha hizo ni za Kennedy Chiguru, Masogo Ndaro, Magina Ng'aranga, Musyangi Kuboja, Muinja Maingu, Benard Merumba, Verynice Masaka, Masatu Julius, Everist Maganga na Evans Mkama.

Wengine ni Profesa Muhongo, Benjamin Mbeba na Bulilo Maingu, huku ikilezwa kuwa bado wapo baadhi ya makada wengine  wanaotarajiwa kuchukua fomu leo au kesho.

Mmoja wa watia nia hao Kennedy Chiguru, amesema miaka ambayo Profesa Muhongo amekuwa mbunge inatosha, na kwamba ni vyema akapumzika na kuwaachia wengine waendeleze pale alipoishia.

"Uongozi ni kupokezana kijiti. Kila mmoja wetu amechukua fomu ili mmojawapo ampokee kijito Profesa Muhongo ambaye amehudumu kwa vipindi viwili tangu mwaka 2015 hadi 2025," amesema Chiguru.

Zoezi la kuchukua fomu hizo lilianza Juni 26 na litaendelea hadi kesho Julai 2 majira ya saa 10 kwa wabunge wa jimbo, ujumbe wa baraza la wawakilishi, ubunge wa viti maalum, ujumbe wa baraza la wawakilishi viti maalum, udiwani wa kata na wa viti maalum.