RC Mboni amuapisha DC mpya wa Kahama

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:04 PM Jul 01 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akimuapisha Mkuu wa wilaya mpya wa Kahama Frank John Mkinda.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akimuapisha Mkuu wa wilaya mpya wa Kahama Frank John Mkinda.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita,amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Mkinda,mara baada ya kuteuliwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Amemuapisha leo Julai 1,2025 kwenye ukumbi wa mikutano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga,hafla iliyohudhuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali,Chama na Taasisi mbalimbali za Serikali, viongozi wa dini na kimila.

Mboni akizungumza mara baada ya kumaliza kumuapisha DC Mkinda,amemuahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha sababu Kahama anaifahamu vizuri na kwamba kabla ya kupanda kuwa Mkuu wa Mkoa,alikuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.

“Nakupongeza kwa kuaminiwa na Rais Samia na kuteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Kahama,mimi nipo na nitakupatia ushirikiano wa kutosha,”amesema Mboni.

Aidha,ametoa maagizo kwa Wakuu wa wilaya wote wa Mkoa huo, kwamba waendelee kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao,pamoja na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua. 

Pia,amewaagiza kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na  ukamilishaji wa maboma ya Zahanati kwa kutumia mapato ya ndani,ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Amewasisitiza kutafuta wawekezaji, ili kuwepo na mzunguko wa fedha na kuinua uchumi wa wananchi wa Shinyanga.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Mkinda,ameahidi kutekeleza maagizo yote aliyopewa,huku akiahidi kudumisha Amani na Utulivu katika wilaya hiyo hasa kwenye kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.

RC UAPISHO 2.jpg 1.46 MB