Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepata utambuzi wa kimataifa kutoka Serikali ya India kama mtoa huduma anayeaminika zaidi.
Hatua hiyo inazidi kuimarisha hadhi yake katika masoko ya nje na pia ATCL imepongezwa kwa kuendesha shughuli zake kwa uwazi, uadilifu, na kwa kuzingatia kikamilifu sheria mbalimbali ikiwemo za kodi.
Utambuzi huo ulitolewa na Wizara ya Fedha ya India kupitia Bodi Kuu ya Kodi za Ndani na Forodha (CBIC), kwa kuzingatia viwango vya juu vya uwajibikaji wa kimataifa pamoja na mchango wa ATCL katika ukuaji wa uchumi wa India kupitia ushirikiano wa kibiashara.
Air Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa mashirika machache ya ndege kutoka Afrika yaliyotekeleza kwa ufanisi masharti mbalimbali, ikiwemo ulipaji wa kodi kwa wakati na kwa uwazi.
Akizungumza kuhusu utambuzi huo, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ATCL, Sarah Reuben alisema, “Tunajivunia kutambuliwa na Serikali ya India, kwani ni moja ya masoko makubwa ya kimataifa yanayojulikana kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa Sheria. Hii ni ishara kwamba Air Tanzania inafuata viwango vya kimataifa na ipo tayari kuhimili ushindani wa soko la kimataifa,” amesema
Amesema kwa sasa, Air Tanzania ina mtandao mpana wa safari za ndani ya nchi, ikihudumia kupitia viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songea, Mtwara, Iringa, Tabora, Kigoma, Bukoba na Zanzibar.
Aidha, amesema Kampuni hiyo inaendesha safari za moja kwa moja za kimataifa kwenda miji mbalimbali ikiwemo Dubai (UAE), Mumbai (India), Guangzhou (China), Johannesburg (Afrika Kusini), Kinshasa na Lubumbashi (DRC), Nairobi (Kenya), Hahaya (Comoro), Ndola na Lusaka (Zambia), Harare (Zimbabwe), Bujumbura (Burundi), na Entebbe (Uganda).
Amesema hivi karibuni, ATCL inatarajia kuzindua safari za moja kwa moja kwenda Lagos, Nigeria, ili kuwaongezea wateja chaguo la safari, kupunguza changamoto za usafiri wa anga katika Afrika Magharibi, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuwaunganisha wananchi kupitia huduma za haraka, salama na za kuaminika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED